Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhadisi Robert Gabriel, leo terehe 26.07.2018 amefanya uzinduzi wa Ujenzi wa Miradi ya Huduma kwa Jamii (CSR) (Ground Breaking Ceremony) inayotekelezwa ndani ya Halmashauri ya Mji wa Geita kupitia fedha za CSR zinazotoka Mgodi wa Dhahabu Geita GGM.
Ujenzi huo ni pamoja na uwekaji wa Mnara kwenye Mzunguko wa Kisasa (Round About) utakaowekewa krasha la kusagia mawe yenye Dhahabu kama alama ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu, saa amabayo pia huonesha nyuzi joto, Mwenge wa Uhuru kama alama ya Taifa, na mfano wa matofali ya dhahabu kama alama ya uwepo wa dhahabu nyingi Mkoani Geita.
Amesema, “tukio hili ni la kihistoria na limeacha alama kwa wanageita kwa kuwa walikua na kiu ya kuona haya yakitekelezeka na kurejesha hadhi ya mkoa”; hivyo ametoa pongezi nyingi kwa Mhe. Rais Magufuli kwa kuweka usimamizi mzuri wa rasilimali za nchi lakini pia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutunga sheria yenye kulinda maslahi ya nchi. Ameushukuru pia mgodi wa GGM kwa ukubali wao wa asilimia mia moja kutekeleza matakwa ya sheria ya madini ya mwaka 2017 kwa kurejesha sehemu ya faida yao kwa jamii kupitia utekelezaji wa miradi na kuomba migodi mingine iige mfano huo, ambapo kwa mwaka huu GGM imetoa jumla ya Shilingi Bilioni Tisa nukta Mbili (Tshs. 9,200,000,000/=) Halmashauri ya Mji ikiwa na mgao wa Shilingi Bilioni Nne nukta Tisa (Tshs 4,900,000,000/=) na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kupata Shilingi Bilioni Nne nukta Tatu (Tshs. 4,300,000,000/=).
Mhandisi Gabriel pia ameweka kwa kuchora alama kwenye eneo lililopo “Iiduka Lise” kama ishara ya kuzindua ujenzi wa vibanda themanini (80) awamu ya kwanza kati ya vibanda zaidi ya mia tatu (300) vinavyotarajiwa kujengwa maeneo ya soko hilo ambalo limejengwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri ya Mji Geita ambalo pia litakuwa na uwezo wa kuegesha magari zaidi ya Sabini (70)
Mwenyekiti wa CCM Mkoa Mhe. Alhaj Said Kalidushi amempongeza Mhandisi Gabriel kwa utendaji kazi wake na amemwambia kandarasi wa vibanda hivyo mwenye jina Magocon Contractor kutoka Dodoma kuwa amepewa jukumu la kutafsiri ndoto na mawazo ya wanageita kwenda kwenye uhalisia na hivyo kama chama hawatapenda kuona anawaangusha. Pia alimtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anafanya kazi kwa kiwango na kwa kuzingatia ubora wa kazi ilia apate fursa ya kupewa miradi mingi Mkoani Geita.
Mkurugenzi wa Mji Geita Mhandisi Modest Apolinary amesema vibanda hivyo vitajengwa kwa gaharama ya Shilingi Bilioni Moja nukta Mbili (Tshs. 1,200,000,000/=) VAT ikiwemo hadi kukamilishwa kwake na kuongeza kuwa tayari wamepata mteja ECO Bank ambaye atatumia eneo la Mita za Mraba Mia Mbili hivyo mkandarasi ajitahidi kukamilisha hata kabla ya muda aliopewa ili kuwapunguzia adha wananchi waliokuwa wakitumia vibanda vilivyokuwepo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita Mhe. Leonard Bugomola ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Bombambili ameshukuru kwa uongozi wa mkoa na Mgodi wa GGM kisha kushauri Mkandarasi kuanza kujenga upande wa mwekezaji ambaye ameonesha nia kuja kukuza uchumi wa Geita yani ECO Bank.
Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini Mhe. Constantine Kanyasu amepongeza juhudi za Mkuu wa Mkoa na GGM na kumsihi mkandarasi ajitahidi kumaliza ujenzi huo kwa wakati ili wananchi waweze kufanya shughuli zao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu GGM Bw.Richard Jordinson amesema ushiriakiano wa Serikali na Mgodi wa GGM unaweka alama kubwa sana kwa wanageita na taifa kwa ujumla hivyo aushukuru uongozi wa Mkoa na Halmshauri za Geita kwa mashirikiano hivyo ni furaha yao kuwa ndoto ya mkoa inatimia na ukamilishwaji wa miradi hiyo mitatu utabadili sura ya Geita.
Mkandarasi alimalizia kwa kuahidi kukamilisha kazi hiyo kabla ya miezi kumi aliyopewa chini ya usimamizi wa Msimamizi Mkuu wa Miradi kutoka GGM Bw. Moses Rusasa japokua Mkuu wa Mkoa pia ameahidi kushirikiana nao kwa usimamizi wa mradi huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa