Kama ilivyo Kauli Mbiu ya Mkoa wa Geita, Amani, Umoja na Kazi vimezidi kudhihirika pale ambapo Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amekutana na kufanya kikao na viongozi wa madhehebu ya dini zote wa Mkoa wa Geita juu ya ufanikishaji wa Maonesho ya kwanza na ya kihistoria ya Teknolojia ya Uchimbaji na Uwekezaji wa Madini ya Dhahabu yatakayofanyika kuanzia tarehe 24-30.09.2018 katika Uwanja wa CCM Kalangalala uliyopo Mjini Geita. Mhe. Mhandisi Gabriel amekutana viomgozi hao tarehe 14.09.2018 katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Lenny iliyopo Mjini Geita.
Akizungumza baada ya kikao kuwekwa wazi na mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maonesho, Mhe. Mhandisi Gabriel aliwaeleza viongozi hao kuwa, maonesho hayo si ya kukosa na kwakuwa ni kwa ajili ya wana Geita, ni dhahili kuwa waumini wanatakiwa kupata habari na taarifa sahihi juu ya tukio hili muhimu ili waweze kushiriki na kwamba yupo tayari kupokea wageni wa kitaifa na kimataifa ambao watashiriki na kutembelea maonesho hayo na kwamba wajiandae kushiriki kikamilifu kwakuwa yameandaliwa vizuri na si ya kukosa.
Amesema, "nipo tayari kupokea wageni, na hii ni katika kuuimarisha uchumi wa Mkoa ikiwa ni pamoja na kuijenga Geita Mpya yenye matumaini makubwa kiuchumi”.
Amewakumbusha viongozi hao kuwaambia waumini waichangamkie fursa hii adhimu iliyopo mbele yao kwakuwa Geita inajengwa na wana Geita wenyewe, hivyo basi ushiriki wao ni muhimu sana kwa ajili ya maonesho hayo yenye kuleta matokeo chanya kiuchumi na kijamii.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Biashara kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi Bi. Twilumba Mlelwa aliwaeleza viongozi hao kuwa, maandalizi ni mazuri hivyo wajiandae kunufaika na mazuri mengi ikiwemo Kongamano litakalojadili fursa na changamoto zilizopo katika Sekta ya Madini, Mikutano ya Biashara (Business to Business) na Semina kwa Wafanyabiashara Wakati n Wadogo. Aidha, kutakuwa na huduma ya Kliniki ya Biashara inayolenga kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili sekta ya biashara nchini.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maonesho na Makamu Mwenyekiti Biashara wa Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Bw. Athanas Inyasi amewashukuru viongozi kwa kuitikia wito na kwa maombi yao yaliyopelekea kuteuliwa kwa Mhe. Mhandisi Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Geita jambo lililowapa faraja kwa kuwa Mkoa kwa sasa unasonga mbele kimaendeleo kutokana na kasi yake ya utendaji kazi. Pia Bw. Inyasi amewaomba viongozi hao kuwahamasisha waumini kushiriki na kupitia mafundisho yao, wafanya biashara waambiwe ukweli kuwa, mafanikio hayaji kwa ushirikina bali kufanya kazi na kutokana na uwepo wa TCCIA na Kliniki ya Biashara kutoka TanTrade, ni vyema kufika na kuwaona wakati wa maonesho ili kupata suluhu na ushauri kwenye biashara zao. Mwisho akawaomba waendelee kumuombea Mhe. Mkuu wa Mkoa na kwa pamoja kuendelea kuijenga Geita na kutegemea maendeleo kwa kasi.
Viongozi wa madhehebu ya dini nao wakaeleza furaha yao kwa namna ambavyo Ofisi ya Mkoa imekuwa ikiwashirikisha katika mambo mbalimbali ya maendeleo na wameahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili Mkoa uendelee kusonga mbele. Pia wamepongeza juhudi za Mkuu wa Mkoa kusogeza huduma mbalimbali za kijamii karibu na wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa