Katika kuuenzi mchango wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baraza la wafanyakazi mkoa wa Geita limetia saini Mkataba wa Baraza la Wafanyakazi uliohusisha Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) pamoja na Sekretarieti ya Mkoa wa Geita jumanne ya Oktoba 13, 2020 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Akifungua kikao cha baraza hilo, mkuu wa mkoa wa Geita mhandisi Robert Gabriel amewaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa, anaiamini timu ya sekretarieti ya mkoa na kwamba itatekeleza mkataba huo kwa ufanisi na ubunifu huku akihimiza mshikamano, kuombeana na kuhurumiana kwani binadamu hukosea.
“mimi ni shemasi wa mkoa huu, ninawaomba watumishi tushikamane, tuhurumiane, tuombeane na tusameheane kwani kukwazana ni sehemu ya maisha”
Mhandisi Gabriel alimaliza kwa kusema kuwa analo deni kubwa kwa watumishi wa sekretarieti ya mkoa wa Geita kwani tangu amekuwa Kiongozi ndani ya mkoa huu, hajawahi kukwazana na mtumishi yeyote hivyo kujiona ana deni la kuwalipa watumishi hao kwa wema wao kwake, kisha kufungua kikao hicho.
Kwa upande wake Ndg.Mgasa Chimola ambaye ni katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) amesema, anaushukuru uongozi wa mkoa kwa maandalizi ya kikao hicho muhimu kuwezesha utiaji saini mkataba huo, jambo ambalo linaonesha msisitizo wa dhana ya ushirikishwaji na mshikamano na kwamba wao kama TUGHE wapo tayari kutoa ushirikiano kwa ofisi ya mkoa katika kuhakikisha wafanyakazi wanazingatia haki na wajibu.
Mganga mkuu wa mkoa Dkt. Japhet Simeo hakuwa mbali kuwasilisha mada inayohusu lishe na kuhimiza watumishi kuzingatia namna bora ya ulaji ikiwa ni utekelezaji wa kampeni iliyoanzishwa na katibu tawala mkoa wa Geita ndg. Denis Bandisa ya kutoa mada mbalimbali kwenye vikao mbalimbali zikiwemo mada kuhusu rushwa, afya, namna ya kujiaandaa kustaafu, ujasiriamali n.k
Akiahirisha kikao hicho, mwenyekiti ambaye pia ni katibu tawala mkoa wa Geita ndg. Denis Bandisa amesema kuwa, watumishi ni vyema kujitahidi kufanya kazi kwa bidii na si kuangalia namna ya kupata vyeo huku akisema, “tujifunze kusikiliza na visivyo tufurahisha” kwa lengo la kuwa tayari kupata elimu ya ziada kisha kuwashukuru wajumbe wa kikao kwa kushiriki na kwa pamoja kuazimia kukutana kwa ajili ya kikao kingine kabla ya maandalizi ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha.
Vikao vya baraza la wafanyakazi hufanyika kufuatia Agizo Na.1 la mwaka 1970 lililotolewa rasmi tarehe 10/2/1970 na Hayati Mwl.Julius Nyerere kupitia dhana ya ushirikishwaji ambayo ni uundwaji wa mabaraza na ili kuweka mkazo, likaimarishwa na Sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Utumishi wa Umma Na.8 ya mwaka 2002 na Kanuni zake za mwaka 2003 kifungu cha 108, Sheria ya Majadiliano Katika Utumishi wa Umma Na.19 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2017.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa