Na Boazi Mazigo – Geita RS
Ikiwa ni mwezi ambao ndani yake ni maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani, mwanafunzi wa kidato cha tatu kutoka shule ya Sekondari Nyanza iliyopo halmashauri ya mji Geita, Bi.Shanti Mahudi (16) ameongoza kikao cha menejimenti ya ofisi ya mkuu wa mkoa Geita ikiwa ni utekelezaji wa programu maalumu inayoratibitibiwa na shirika lisilo la kiserikali la Plan International Tanzania ijulukanayo kama Girls Takeover, programu ambayo hufanyika kwa kumwezesha msichana kuwa kiongozi ndani ya muda mchache akiigiza kutekeleza majukumu ya kiongozi husika kwa lengo la kumjengea uwezo na ujasiri.
Bi.Shanti ameongoza kikao hicho Oktoba 19, 2023 katika ofisi ya Katibu Tawala Mkoa ambapo ameketi na wakuu wa idara na vitengo mbalimbali akizungumza nao akisisitiza juu ya uzingatiaji mahitaji maalumu ya mtoto wa kike kwenye shule zote ikiwemo maji safi na salama, taulo za kike (Sodo) pamoja na chumba maalum cha kujihifadhi mabinti wanapokuwa kwenye siku zao za hedhi n.k.
“niwashukuru kwa mwitikio wenu na niombe muwasaidie wasichana kupata maji safi na salama, ulinzi, taulo za kike (sodo). Mtambue yakuwa, watoto wa kike wanapotoka nyumbani kuelekea shule, hukutana na vishawishi vingi njiani, hivyo ni muhimu kuwaongezea ulinzi kwa kujenga mabweni kwenye shule”, alisema Bi.Shanti.
Bi.Shanti alihitimisha kwa kusisitiza juu ya uendelezwaji vipaji kwa watoto wa kike ikiwemo kuwajengea vyumba maalum bila kusahau waalimu wenye vipaji na upatikanaji wa vifaa vya michezo. Aidha, aliomba viongozi kusaidia kuondoa mtazamo hasi unaomtafsiri mtoto wa kike kama hastaili kupewa elimu bali wasaidiwe kupata elimu kwakuwa nao wana mchango mkubwa ikiwemo kuwa viongozi wakubwa nchini.
Kwaniaba ya menejimenti ya ofisi ya mkuu wa mkoa Dkt.Omary Sukari ambaye ni kaimu katibu tawala mkoa alisema, yote yaliyosemwa na Bi.Mahundi yatashughulikiwa na yamekuwa yakipewa msukumo kuanzia ngazi ya mkoa hadi halmashauri huku akisema, “nikushukuru kwa ziara yako, na nikuhakikishie yote uliyotueleza kila mmoja kwenye nafasi yake ataenda kuyatekeleza; na nichukue fursa hii kumpongeza mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwarejesha watoto wa kike waliopata ujauzito wakiwa masomoni na kama mkoa tutaendelea kumhakikishia mtoto wa kike ulinzi ili aweze kusoma na kufikia malengo yake”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa