Katibu Tawala Mkoa wa Geita Ndugu Mohamed Gombati ameagiza uongozi wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita kufanya kazi kwa weledi na kushirikiana na Timu ya Menejimenti ya Hospitali hiyo ili kufikia malengo makuu ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi bila mikwamo yoyote.
Ndg. Mohamed Gombati ametoa rai hiyo alipokuwa akiizindua rasmi Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita tarehe 12 Februari 2025 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita ameeleza kuwa kazi kubwa ya Bodi ni kusimamia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya Timu ya Menejimenti ya Hospitali, hivyo ni chombo muhimu sana katika uendeshaji wa huduma zinazotolewa hospitalini hapo na pia ni daraja linalowaunganisha wananchi na Serikali kupitia huduma zinazotolewa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
“ndugu zangu fanyeni kazi kwa bidii, maarifa na uaminifu mkubwa ili kuacha kumbukumbu ya kazi nzuri mtakayoifanya kwenye historia ya Hospitali yetu ya Mkoa, kwa niaba ya Serikali ya Mkoa wa Geita nawaahidi kuwapa ushirikiano wajumbe wote wa Bodi teule kwa kipindi cha miaka mitatu mtakayokuwa kwenye uongozi.” Aliongeza Ndg. Mohamed Gombati.
Ndg. Mohamed Gombati ametumia fursa hiyo kutoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa ujumla kwa kuendelea kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma bora za afya kwa kujenga majengo mbalimbali, kusambaza dawa na vifaa tiba pamoja na kuleta wataalam katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vilivyoko ndani ya Mkoa wa Geita.
Mwenyekiti mpya wa Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita Wakili Manase Ndoroma ametoa shukrani za dhati kwa Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuwaamini na kuwateua kuwa wasimamizi wa Hospitali hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu na kuahidi kutekeleza majukumu waliyokasimiwa kwa ufasaha ili wananchi waweze kuendelea kupata huduma bora za afya.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Fadhili Kibaya amewaasa wajumbe wa Bodi hiyo kufanya kazi kwa umoja kama timu ili waweze kutimiza wajibu wao kwa ufanisi wakitambua kuwa wananchi wa Mkoa wa Geita wanahitaji kupata huduma bora kupitia usimamizi wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt. Omari Sukari amewapongeza wajumbe wa Bodi kwa kuteuliwa kuwa wawakilishi wa wananchi katika usimamizi wa huduma za afya zinazotolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita na kuwaasa kutumia nafasi hiyo vizuri ili matarajio ya wananchi katika upatikanaji wa huduma bora za afya yaweze kufikiwa.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita ilianza kutoa huduma Mwezi Juni 2016 baada ya Wizara ya Afya kuipa hadhi ya kutoa huduma za rufaa kwa Mkoa pamoja na kusaidia vituo vya Afya katika ngazi za chini na Taasisi za mafunzo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa