BUCKREEF GOLD COMPANY LIMITED WATAKIWA KULIPA FIDIA GEITA
Kampuni ya Uchimbaji wa Madini ya Dhahabu Buckreef Gold Limited imeagizwa kufanya utaratibu wa kulipa fidia kwa wananchi wanaozunguka mgodi huo kabla ya kuanza uzalishaji.
Akizungumza katika eneo la Kampuni hiyo iliyopo Lwamgasa Wilaya ya Geita Waziri wa Madini Mheshimiwa Angella Kairuki amesema kuwa ni vizuri kampuni hiyo ikaanza utaratibu wa kuandaa fidia kwa ajili ya wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa ili kufanya kazi katika eneo hilo kwa amani.
Amesema kuwa zoezi hilo lilishindwa kutekelezeka baada ya kampuni hiyo kutokubaliana na idadi kubwa ya wananchi ambao walifikia 1062 baada ya usamini kufanyika. "Serikali kupitia Wizara ya Madini na Wizara ya Ardhi zitaleta wataalamu ili kufanya tathimini hiyo kwa dharula ili kujiridhisha na Idadi hiyo na baadae kuendelea na taratibu za fidia kabla ya kuendelea na hatua zingine". Mgodi wa Buckreef unamilikiwa na Serikali kupitia STAMICO pamoja na Buckreef Gold Limited kupitia TANZAM.
Katika Hatua zingine Waziri wa Madini ametembelea Mgodi wa Busolwa Mine ambao unamilikiwa na mwekezaji mzawa na kupongeza juhudi zinazofanywa na kampuni hiyo kwa kulipa kodi pamoja na kutoa huduma za jamii kwa maeneo ya jirani. Ametoa wito kwa watanzania wengine wenye uwezo wa kufanya shughuli za uchimbaji wa madini kujitokeza ili kufanya kazi hiyo kwa kuwa Serikali inaunga mkono wawekezaji wa ndani.Mgodi wa Busolwa Mine unathamani ya dolla milioni 25.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa