Ni mwendelezo wa Mabaraza Maalum Kujadili hoja za mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali CAG kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni, 2018 ambapo mkuu wa mkoa wa geita mhandisi Robert Gabriel ameendesha mkutano huo maalum wa kujadili taarifa kutoka kwa CAG Julai 17, 2019 katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya wilaya ya chato
Akiongea wakati wa kuhitimisha mkutano huo, mhandisi Gabriel ameagiza kujibiwa mapema kwa hoja ambazo hazijajibiwa ndani ya wiki mbili huku akieleza mambo kadha ambayo halmashauri hiyo inapaswa kuyafanya katika kuhakikisha inaendelea kupata hati inayoridhisha au iliyo safi.
“ni muhimu wakaguzi wa ndani kuhakikisha wanatoa taarifa endapo mtaona viashiria vya hoja, menejimenti epukeni usiri, fedha yote inayoingia hakikisheni madiwani wanapata taarifa na miongozo ya matumizi ya fedha hizo yanawekwa wazi kupitia miongozo inayoletwa. Vilevile hakikisheni hamuingii mikataba na wakusanya mapato msiowajua lakini msiwaache wakae na makusanyo/fedha kwa kipindi kirefu. Pia kama mkoa, tumekubaliana tutafanya kaguzi kila robo na kuchukua hatua pale itakapobidi ili tusipate hoja”, alisema Mhandisi Gabriel.
Mhandisi Gabriel amempongeza katibu tawala mkoa Denis Bandisa kwa namna anavyoendelea kuwajengea uwezo watumishi ndani ya mkoa na kusisitiza halmashauri hiyo kukusanya mapato kwa kushirikiana ili hata kuweza kutekeleza miradi na kulipa malipo ya watoa huduma ili kuepusha manung’uniko na kumaliza akisema, “hakuna mafanikio bila kufanya kazi kwa umoja”.
Mustafa Saidi kwaniaba ya mkaguzi mkuu wa nje ameeleza kuwa, katika mwaka wa fedha unaoishia juni 2018, halmashauri ya chato imepata hati inayoridhisha “Unqualified Opinion” na kuwapongeza watumishi wake kwa ushirikiano ambao huwa wanautoa kwa wakaguzi kila mara wanapofanya shughuli hiyo ya kujibu hoja.
Mkaguzi Saidi amesema “utekelezaji wa maoni ya CAG ni wa kuridhisha kwakuwa kati ya hoja 46 zilizotolewa kwa hesabu za 2017/2018 zikijumuisha hoja za miaka ya nyuma ni hoja 33 tu ndizo zimepatiwa majibu ya kuridhisha na kufungwa na hivyo kusalia na hoja 13 sawa na 28%”
Ameendelea kubainisha kuwa, hoja zilizosalia, zimegawanyika katika makundi 2 ya hoja ambazo zimepatiwa majibu yasiyoridhisha na hoja ambazo zimepatiwa majibu lakini bado zinaendelea kutekelezwa hivyo zimesalia kwaajili ya ufuatiliaji.
Kwa upande wake katibu tawala mkoa Denis Bandisa amesema, bado halmashauri hii inatakiwa kuongeza jitihada akitoa mfano wa halmashauri ya mji geita yenye hoja 4 tu hivyo ni muhimu kuzingatia ushauri uliotolewa ili kupunguza hoja hizo, hivyo kuelekeza kujibu kwa wakati.
Mwisho Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Christian Manunga akatoa ahadi kwa mkuu wa mkoa ya kuwasilisha majibu mapema lakini pia kutekeleza ushauri na maelekezo yote yaliyotolewa huku akiwasihi madiwani pamoja na watalaam kuendelea kutoa ushirikiano ili isitokee hata siku moja wakapata hati chafu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa