Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Hashim Komba amezindua rasmi Maonesho ya saba ya Siku ya wakulima Duniani ( Nanenane) Kanda ya ziwa magharibi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela.
Akizindua Maonesho hayo Mhe. Komba amewahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kufika katika maonesho hayo ili kuona na kujifunza maboresho yenye ubunifu mkubwa wa uzalishaji katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi.
“Wananchi tembeleeni mabanda yote ambayo yanajihusisha na sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ili mpate ujuzi, maarifa na teknolojia iliyoboreshwa, ukuaji wa teknolojia utawawezesha wananchi kufanya shughuli zenye tija katika sekta wanazofanyia kazi na kukuza uchumi na uzalishaji.” Aliongeza Mhe. Hashim Komba.
Aidha Mhe.Komba amewataka wananchi kujifunza kilimo cha eneo dogo chenye tija huku akiwasihi kujipanga na kuchukua mikopo yenye tija kutoka taasisi mbalimbali za kifedha zinazoshiriki ili kukuza vipato vyao katika shughuli wanazojighulisha nazo.
Sambamba na hayo Mkuu wa Wilaya ya Geita amegusia kauli mbiu ya Maonesho hayo isemayo “Chagua viongozi bora kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi 2025” kwa kutoa Rai kwa wananchi kujiandaa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29 ,2025 huku akitaja sifa za kiongozi bora kuwa ni mwenye kujua ubunifu mkubwa wa kugusa maisha ya watu wengi.
Mhe. Komba ametoa rai kwa mamlaka za Serikali za Mitaa kuona umuhimu wa kutumia vyema mikopo inayotolewa na Halmashauri kutoa kipaumbele cha kuwapatia mikopo vikundi vinavyojishughulisha na sekta za uzalishaji kwa sababu Zaidi ya asilimia 70 sekta hizo zimetoa ajira kwa wananchi. Pia Taasisi za kifedha toeni mikopo yenye riba nafuu kwa wananchi wanaotafuta uwezeshwaji katika kuendeleza na kuzalisha Zaidi katika sekta hizo.
Mwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Mwanza ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe CDE.Christopher E.Ngubiagai amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha na kuendelea kuwekeza katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi ikiwa sehemu ya kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi
Akisoma taarifa ya maonesho hayo Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Mwanza Ndg. Peter Kasele amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la washiriki kila mwaka hali inayoonyesha utayari wa watu katika kujifunza na kupokea vitu vipya.
Maonesho ya wakulima nane nane kanda ya ziwa magharibi yanahusisha mikoa miwili ya Mwanza na Geita.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa