Katika kufanikisha Azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhusu kuboresha Elimu, zaidi ya shilingi za kitanzania Bilioni 6.8 zimetolewa na Serikali zilizowezesha uchapishaji wa nakala 3,583,750 zitakazosambazwa nchi nzima hadi kufikia mwezi Januari, 2019.
Akizundua zoezi hilo lililofanyika tarehe 22.12.2018 katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Nyankumbu iliyopo Mjini Geita, Dkt. Avemaria Semakafu, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwaniaba ya Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (Mb) Waziri mwenye dhamana na Elimu amesema, viongozi wanaosimamia elimu, wanao wajibu wa kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa kwa asilimia zote lakini pia wahakikishe lengo la usambazi wa vitabu hivyo linafikiwa huku akiipongeza Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa jinsi walivyofanikisha utoaji wa vitabu mbambali ikiwemo vya darasa la pili, la tatu, la nne na vya la tano.
Amesema, “kwanza namshukuru Mhe.Rais kwa kutoa fedha za kufanyia shughuli hii, lakini pia niipotengeze TET kwa namna walivyofanya kazi hii kwa moyo na kuifanikisha na niwashukuru Geita kwa kunipokea”.
Dkt. Semakafu ameeleza kuwa, ni matarijio yake kuwa hadi kufikia Januari 7, 2019 vitabu vyote vitakuwa vimefika au kuwa katika hatua ya mbali ya usambazaji, huku akiwataka Maafisa Elimu na Wathibiti Ubora kwa pamoja wahakikishe vitabu vinafika mashuleni na vinapokelewa kwa mujibu wa taratibu za mapokezi, vinatumika na wanafunzi kwani vitabu kuwa vipya siyo sifa nzuri bali vyatakiwa kusomwa hata lengo lionekane kutimia.
Ameongeza kufafanua kuwa “vitabu hivi ni kwaajili ya darasa la tano mwaka 2019, hivyo walio madarasa ya mbele havitawahusu na kwamba huu ndiyo utaratibu wa kuondoa mtaala wa zamani.”
Amewataka wanafunzi kudai kupata vitabu ili wajisomee huku akisisitiza kuwa ni vyema vitabu hivyo ambavyo uwiano wake ni kitabu 1 kwa wanafunzi 3, viandikwe majina ya hao watakaovitumia na kwamba vinaposomwa vitabu hivyo, vitampa mwanafunzi uweo wa kuwa na ufahamu, udadisi, umakini na kumwezesha kupata maswali ya ziada kumuliza mwalimu. Na katika hili amewaambiwa walimu kuwa, wanapaswa kujiandaa kujibu ama kutoa ufafanuzi kwa wanafunzi, lakini wao kama walimu wasikae na changamoto wanapokutana nazo bali waziwasilishe kwa waratibu elimu kata, maafisa elimu wilaya na wathibiti ubora, kwamba kwa namna hiyo watafanikiwa.
Ameupongeza uongozi wa serikali ya mkoa kupitia wawakilishi Bw. Denis Bandisa, Katibu Tawala Mkoa na Mwl. Shaban Kamchacho ambaye ni Afisa Elimu Mkoa kwa jitihada za kutatua changamoto ya uhaba wa miundombinu ya madarasa kwa kuwa na zaidi ya madarasa 8,000 yaliyo katika hatua mbalimbali za ujenzi, kisha kutangaza uzinduzi wa zoezi la usambazaji
Awali Dkt. Aneth Komba, Mkurugenzi Mkuu TET akisoma taarifa fupi ya kazi ya uandishi na usambazaji wa vitabu vya darasa la tano, amesema vitabu hivyo vinajumuisha masomo nane ambayo ni Hisabati, Kiingereza, Kiswahili, Stadi za Kazi, Maarifa ya Jamii, Sayansi na Teknolojia, Uraia na Maadili pamoja na Kifaransa na kwamba katika usambazaji wake, tayari zimeundwa kamati ya usambazaji hivyo ni tumaini la taasisi kwamba vitabu hivyo vitafika havitabaki maofisini kwa wakuu wa shule na kwenye halmashauri.
Akitoa neno fupi, Bw. Benjamin Oganga, Mkurugenzi Msaidizi, Elimu Sekondari kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI amewapongeza TET kwa namna ilivyofanikisha lakini pia kuwaasa viongozi kufuata maelekezo yote wakidumisha ushirikiano wanapotekeleza majukumu hayo.
Katika kuhitimisha, Prof. Benadetha Kilian na Mwenyekiti wa Bodi ya TET, alitoa neno la shukrani huku akiwahamasisha wanafunzi kusoma kwa bidii ili nao waweze kufikia kiwango cha juu cha elimu wakilisaidia taifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa