Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kwa kanisa na waumini wa dhehebu la Katoliki mjini Geita kufuatia tukio lililotokea usiku wa kuamkia tarehe 26 Februari, 2023 ambalo lilimhusisha kijana mmoja wa kiume ambaye alivunja sehemu ya mlango yenye kioo na kuingia katika kanisa kuu la kiaskofu jimbo kuu Katoliki mjini Geita kisha kufanya uharibifu wa vitu pamoja vifaa vya kuendeshea ibada.
Salaam hizo zimewasilishwa Machi 1, 2023 na mkuu wa mkoa Geita Mhe.Martine Shigela alipofika na kumtembelea Askofu Mkuu jimbo kuu Katoliki Geita Flavian Kassala kisha kutembelea na kujionea maeneo yote ndani ya kanisa yaliyofanyiwa uharibifu kisha kuwasilisha salam za mhe.Rais huku akionesha kusikitishwa na kitendo hicho.
“nimekuja kulaani kitendo kilichofanywa na kijana huyo, lakini pia mheshimiwa Rais wetu dkt.Samia Suluhu Hassan anatoa pole nyingi kwako binafsi, kwa kanisa na waumini wote na ninakuhakikishia ushirikiano kutoka serikalini na jeshi la polisi linaendelea na upelelezi na pindi utakapokamilika wahusika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria. Pia nikuahidi tarehe 18 Machi tutakuja kushiriki pamoja kufungua ibada upya baada ya taratibu zenu kukamilika”. Alisema RC Shigela.
Akishukuru kwaniaba ya kanisa, Askofu wa jimbo kuu Katoliki Geita Flavian Kassala alisema “tunaendelea kutoa shukrani kwa serikali na hasa kupitia vyombo vyake, kwani tulipowaarifu tumepata tatizo, mlijibu mara moja na kutuletea ulinzi. Matumaini makubwa ya watu na jamii kwa ujumla juu ya suala hili yapo kwenu na kwa kuzingatia tafsiri zaweza kuwa mbalimbali”.
Vilevile, Askofu Kassala alimaliza kwa kumshukuru Mhe.Rais akisema wamepokea salamu huku akiongeza “uovu huu unatufanya kuelewa ni aina gani ya jamii tuliyonayo hivi sasa na kwa maana hiyo, ipo haja ya kusaidia ama kuwekeza kwenye malezi hasa kwa vijana”
Mwisho, kamanda wa jeshi la polisi mkoani Geita Safia Jongo alisema kuwa, bado jeshi linaendelea na uchuguzi ili kupata kiini hasa cha jambo hilo hivyo kutoa rai kwa wananchi kuwa na subira na kwamba si vyema kulihusisha jambo hilo na masuala ya chuki baina ya mtu au madhehebu bali kusubiri majibu ya uchunguzi.
Itakumbukwa kuwa baada ya tukio hilo, Askofu Kassala alitangaza kufungwa kwa muda maalum wa siku 20 kwa kanisa kuu la kiaskofu la jimbo katoliki la Geita ili kulitakatifuza kanisa hili ili liendelee kutoa huduma hiyo na kwamba waumini kwa sasa wametakiwa kusali kwenye maeneo yaliyo jirani nao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa