Katibu Tawala Msaidizi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Bw. Herman Matemu, amesema kuwa mafunzo ya mfumo wa e-Mrejesho yaliyotolewa kwa waratibu wa Mfumo huo ndani ya Mkoa wa Geita yatawasaidia wananchi kufikisha kwa urahisi malalamiko na changamoto wanazokumbana nazo pindi wanapokuwa wanapokea huduma kutoka katika Taasisi za Serikali.
Akifunga mafunzo hayo ya mfumo wa Mrejesho kwa waratibu wa Mfumo huo kutoka katika Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Hospitali za Wilaya, Mkoa na Kanda pamoja na Halmashauri za Wilaya na Manispaa hivi karibuni, Ndugu Herman Matemu kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita amesema kuwa kupitia mafunzo hayo, wananchi na watumishi watapata uelewa wa namna ya kutumia mfumo huo wa kidijitali kuwasilisha maoni, maulizo malalamiko na mapendekezo yao kwa wakati, hatua ambayo itaweza kuisaidia kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza uwajibikaji kwa watumishi katika taasisi anazizisimamia.
Ndg. Herman Matemu ametoa wito kwa Waratibu wote waliopatiwa mafunzo hayo kuhakikisha kuwa changamoto zote zitakazowasilishwa kutoka kwa Wananchi zinajibiwa kwa wakati na kwa haraka. Sambamba na hilo amewasisitiza Waratibu wa Mfumo huo pamoja na watumishi wa Umma katika Mkoa wa Geita kutumia lugha ya staha na heshima katika utoaji wa huduma kwa Wananchi
Afisa Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bibi Nasra Kasimu Idury, amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo yanalenga kuhakikisha taasisi za umma zinapokea, zinashughulikia na kutatua malalamiko ya wananchi kwa ufanisi na kwa wakati.
Bi. Nasra Kasimu ameongeza kuwa mafunzo hayo pia yanakusudia kuimarisha utekelezaji wa mwongozo wa mrejesho wa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na Serikali, ili kuongeza uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.
E-mrejesho ni mfumo wa kielektroniki wa kutuma, kupokea na kufuatilia malalmiko, mapendekezo, maulizo na pongezi kuhusu huduma zinazotolewa na Serikali
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa