Katibu Tawala Mkoa wa Geita Ndugu Mohamed Gombati amewataka watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita kudhibiti mianya ya udokozi na utoroshaji wa mapato ya Serikali na kuepuka kuhujumu jitihada za makusanyo ya mapato ya Halmashauri.
Ndg. Gombati ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Geita katika kikao kazi kilichofanyika tarehe 30 Juni 2025 kwenye ukumbi wa mikutano katika Viwanja vya Maonesho vya Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan Bombambili, Geita mjini.
Katibu Tawala Mkoa wa Geita ameeleza kuwa watumishi wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu ambao wanahusika na ukusanyaji mapato waepukane na tabia ya kutoa siri ya mikakati ya ukusanyaji mapato iliyowekwa na Serikali Pamoja na kuachana na desturi ya kuomba rushwa kwa wananchi wakati wa utoaji huduma.
Sambamba na hilo Ndg. Mohamed Gombati amewakumbusha watumishi hao kufanya kazi kwa upendo, umoja na ushirikiano pasipo kusahau kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za utumishi wa Umma Pamoja na kusimamia misingi ya utawala bora na maadili ya Utumishi wa Umma.
“Watumishi wenzangu mnatakiwa kutambua kuwa kila mmoja wenu kulingana na kada yake ni mtu muhimu katika kuhakikisha shughuli za Serikali zinafanywa kikamilifu na kwa kuheshimiana pasipo kusahahu viapo vya kazi na utunzaji wa siri za ofisi kwa lengo la kuongeza umakini wa kazi Pamoja na kuiwezesha Halmashauri kutimiza vyema majukumu yao”. Aliongeza Katibu Tawala Mkoa wa Geita.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita Ndg. Yefred Myenzi ametoa shukrani za dhati kwa Katibu Tawala Mkoa kwa kuketi Pamoja na watumishi wake katika kikao ambacho kimetoa fursa kwa watumishi wote kutoa changamoto na ushauri unaolenga kuboresha utendaji kazi na kusaidia kuchochea maendeleo ya Manispaa ya Geita na Mkoa wote kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa