Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa suluhu ya mambo mbalimbali ili kuongeza ufanisi wa shughuli ikiwemo upande wa sekta ya madini.
Hayo yalibainika Agosti 10, 2023 wakati mkuu wa mkoa Geita mhe.Martine Shigela akifungua kikao maalum kwa ajili ya kuelimishana juu ya Kanuni za wajibu wa wamiliki wa leseni za madini kwa jamii CSR za mwaka 2023 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa Geita.
Akizungumza kabla ya ufunguzi wa kikao na baada ya majadiliano, RC Shigela alisema, “tunaipongeza serikali chini ya Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa kanuni hizi, lakini pongezi nyingine zimfikie waziri wa madini Mhe.Dkt.Doto Biteko pamoja na wizara kwa jitihada hadi leo ili kutatua changamoto za upatikanaji wa kanuni za CSR. Ni matarajio yangu kuwa mpango wa CSR mwaka 2024 utazingatia kanuni hizi”.
RC Shigela aliongeza kwa kumpongeza katibu tawala mkoa Prof.Godius Kahyarara pamoja na mgodi wa GGML kwa kushirikiana kuandaa kikao hicho, kisha kuwasihi washiriki wa kikao hicho kuanza mara moja matumizi ya kanuni hizo na kwamba endapo changamoto zitajitokeza, kanuni hizo zitaboreshwa zaidi.
Naye mwenyekiti wa CCM mkoa Geita Nicholaus Kasendamila alisema,”ninawashukuru wote wenye uchungu na Geita yetu. Kanuni hizi zikatusaidie kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zatukabili”.
Akiwasilisha kanuni hizo, afisa biashara madini mwandamizi idara ya ukaguzi, biashara ya madini, ushirikishwaji wa Watanzania na CSR bw.Issa Lunda alisema, miongoni mwa kanuni hizo ni ile ambayo 40% itatengwa kwa ajili ya miradi ya kijiji au mtaa ambapo shughuli za madini zinafanyika na 60% itatengwa kwa ajili ya miradi ya halmashauri ya wilaya, mjin manispaa au jiji husika ambako shughuli za madini zinafanyika.
Bw.Lunda aliongeza kuwa ni muhimu CSR kuzingatia kubadilisha maisha ya wananchi walio maeneo yaliyo na uchimbaji akitolea mfano wa kuhama kwenye kilimo cha umwagiliaji kuliko kutegemea mvua. Alihimiza uaminifu na uadilifu kwa maofisa wanaosimamia CSR ili kuleta tija kwa wananchi huku akiainisha changamoto ambazo zilikuwa zinatokana na kutokuwa na kanuni kama miradi kutotekelezwa kwa wakati, kupishana kwa mtazamo kati ya halmashauri na migodi pamoja na uelewa mdogo wa masuala ya CSR.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe wakiwemo wajumbe wa kamati ya usalama mkoa, sekretarieti ya mkoa, wabunge, kamati ya usalama wilaya, madiwani, watendaji kata pamoja na wakuu wa idara halmashauri ya wilaya ambapo Agosti 11, 2023 ni zamu ya halmashauri ya mji Geita zote zikiwa wilaya ya Geita.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa