Na Boazi Mazigo-Geita
Katika kuhakikisha jamii ya mkoa wa Geita inalindwa dhidi ya mlipuko wa magonjwa mbalimbali, imeshauriwa kuwa ni muhimu kuchukua tahadhari zote ikiwemo kudumisha usafi wa mwili na mazingira ili kujikinga na ugonjwa wa Homa ya virusi vya Marburg ambao umeripotiwa kuingia nchini hivi karibuni kupitia mkoa wa Kagera.
Hayo yameelezwa Aprili 5, 2023 na Kaimu Katibu Tawala Mkoa Geita Bw.Deodatus Kayango wakati akifungua kikao cha Kamati ya Uelimishaji na Ushirikishwaji wa Jamii ya Kupambana na Magonjwa ya Mlipuko (RCCE) katika ukumbi wa mikutano ofisi ya mkuu wa mkoa Geita huku pamoja na mbinu nyingine akiwataka wajumbe kuwa mabalozi wa kuuelimisha umma juu ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo kwani hauna tiba hadi hivi sasa.
“ninyi ndiyo mabalozi wa kujikinga na Marburg, tukahamasishe usafi, tutumie vyombo vya habari, wasanii watunge mashairi, twende kwenye vyuo na shule kote tufikishe elimu hii. Tahadhari ni bora kuliko tiba, hivyo kwa pamoja tunaweza kuikoa jamii tukitambua kwamba, mpaka sasa mkoa wetu haujapata mgonjwa wa Marburg na tunaendelea kuimarisha utoaji elimu na ufuatiliaji wa wahisiwa kwa umakini”. Alisema Kayango
Bw.Kayango aliongeza kuwa, kwa kuzingatia kuwa mkoa huu upo jirani na mkoa wa Kagera, tayari umeandaa na kusimamia uwepo wa timu za kitaalamu kukabiliana na milipuko ngazi ya Mkoa na Halmashauri na kwamba timu hizo ziko tayari kukabiliana na ugonjwa huu. Vilevile, mkoa utafanya taratibu zote za uchukuaji sampuli kwa wahisiwa pale watakapopatikana kuwa na dalili za ugonjwa huo.
Awali akitoa neno la utangulizi, mganga mkuu mkoa Geita Dkt.Omari Sukari alisema, kufuatia uthibitisho wa uwepo wa homa ya Marburg mkoani Kagera kupitia wizara ya afya na kwakuwa sisi ni mkoa jirani ndiyo maana ni muhimu kujipanga na kuchukua tahadhari kwa kupeana elimu na kuhusisha wadau mbalimbali, hivyo tahadhari zilizotumika wakati wa CORONA kama kunawa mikono pamoja na kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono ni muhimu sana.
Naye mwenyekiti wa CCM Mkoa Geita Mhe.Nicholaus Kasendamila alisema, yupo tayari kueneza elimu ya kujikinga na ugonjwa huo kupitia mikutano ya CCM kwa kutoa muda wa awali kabla ya kuanza vikao vyao.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa msaafu Mhandisi Robert Gabriel akitoa neno la shukran kwaniaba ya wajumbe wa kamati hiyo alisema, anampongeza sana Rais wa awamu ya Sita Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya afya katika kipindi hiki na kuwasihi wajumbe kutumia fursa hiyo kukabiliana na ugonjwa huo hatari na kwamba wako tayari kutumika na watakuwa mstari wa mbele kwenda misikitini, makanisani,kwenye vyombo vya habari, kwenye shule, maeneo ya hadhara n.k ili kutoa elimu waliyoipata.
Mwisho, kwaniaba ya wadau wa maendeleo mkoani Geita , Meneja wa Plan International Geita Bw.William Mtukananje alisema, “iumepewa jukumu kubwa, ni lazima tulifanye kwa kadri tunavyoweza kwani ikiwa hakuna jamii iliyosalama hata sisi hatutaweza kufanya majukumu yetu na tutashirikiana na serikali yetu”.
Ikumbukwe kuwa, Virusi vya Marburg ni ugonjwa hatari wa mlipuko unaosababishwa na virusi vya Marburg. Virusi hivi kwa mara ya kwanza viligundulika mwaka 1967 katika mji wa Marburg huko Ujerumani na miongoni mwa mataifa ya Afrika ambayo yamewahi kukumbwa na ugonjwa huu ni pamoja na Angola, Kongo ,Kenya, Afrika kusini, Zimbabwe na Uganda na kwa wastani virusi huua nusu ya walioambukizwa
Tarehe 21 Machi, 2023 Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalim alitangaza kuwepo kwa ugonjwa huu Bukoba vijijini ambapo watu 8 waligundulika kuwa na Marburg na watu 5 kati yao walifariki wakiwemo watoa huduma za afya.
Kwakuwa ugonjwa huu hauna tiba maalumu wala chanjo, ni muhimu kuzingatia uonapo dalili zake ambazo ni homa, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, kuharisha, mwili kuishiwa nguvu, vidonda vya koo, vipele vya ngozi, maumivu ya tumbo, kutapika, kutokwa damu sehemu za wazi kama vile puani, kutapika damu na kuharisha damu, toa taarifa kwa uongozi uliopo ili kupata timu ya wataalamu waliofundishwa kumhudumia mshukiwa wa virusi hivi.
Geita Bila Marburg Inawezekana, Chukua Tahadhari
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa