Mkuu wa mkoa wa Geita, Mhe. Rosemary Senyamule amewataka viongozi wa dini pamoja na viongozi wa siasa kushirikiana kwa pamoja kuwaunganisha watanzania kwa lengo la kudumisha amani na mshikamano uliopo nchini kama tunu ya taifa.
Amesema hayo Leo tarehe 08.desemba 2021 wakati akiwaongoza wananchi wa mkoa wa Geita kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru na 59 ya Jamhuri hafra hiyo imefanyika katika ukumbi wa GEDECO mjini Geita amewataka viongozi kuwaunganisha watanzania ili kulinda umoja na mshikamano uliopo nchini kama tunu ya taifa ili kuenzi amani na mshikamano uliopo nchini.
Aidha, Mhe. Mkuu ametoa wito kwa wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kwalengo la kujiletea maendeleo.
"Nitoe wito kwenu kila mmoja afanye kazi kama vile atakufa leo, ili uhuru huu uendelee kuleta maana na kuonesha thamani ni maendeleo hivyo kila mtu afanye kazi kwa kujituma kwa bidii kwani uchumi haukuwi kwa kulala usingizi",amesema.
Vilevile, Mhe. Senyamule amesema baada ya baba wa Taifa viongozi waliofuata waliendelea kuboresha Miundombinu ya barabara na huduma zingine za kutolea huduma za afya kwa wananchi kwa lengo la kukuza uchumi wa taifa.
Hata hivyo mkuu wa mkoa amewapongeza wananchi wa Geita kwa kuishi kwa kudumisha amani. "Historia inaonesha miaka michache iliyopita Geita haikua salama kutokana na matukio ya mauaji ya vikongwe na albino lakini sasa mkoa upo salama hivyo tuendelee kuienzi amani na tukatae kujiingiza kwenye matendo yote yanayohatarisha amani ya nchi." Amesema.
Vile vile Mhe Mkuu wa Mkoa wa Geita amewataka wananchi wa mkoa huo kusimamia na kuelimisha wananchi kwa lengo la kuchukua tahadhari kwa kutunza mazingira pamoja na kuhifadhi vyanzo vya maji ili kuondokana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi.
Hata hivyo chanjo ya hiyari ya Ugonjwa wa Uviko 19 ameigusia na ametoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa ya kuchanja kwa hiyari ili kujikinga na maradhi hayo ambayo hivi sasa tupo kwenye wimbi la nne la ugonjwa huo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe, Wilson Shimo ametumia nafasi hiyo kwakuwataka wananchi kudumisha umoja pamoja na kufanya kazi kwa bidii kama ngao ya kujitegemea kwenye wakati huu ambapo Taifa limefikisha miaka 60 ya Uhuru.
"Akina mama wanakopesheka maana wanaongoza kwa urejeshaji wa mikopo kwenye Halmashauri haya ni matunda ya Uhuru wa Tanzania." Mhe. Martha Mkupasi Mkuu wa Wilaya ya Chato.
Aidha, Mhe. Mkupasi amesema kuwa kuelekea Miaka 60 ya Uhuru nchini, kumekua na ongezeko la viongozi wanawake na akabainisha kuwa akinamama ni nguzo imara na ndio viongozi kwenye ngazi za familia.
Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Mhe. Mhandisi Charles Kabeho amesema hali ya usafiri zamani ilikua ya shida lakini kwa sasa watu wanasafiri kwa urahisi kutokana na kuimarishwa kwa Miundombinu hapa nchini.
"Kila mtanzania ana wajibu wa kufikiri ana wajibu gani wa kulitumikia Taifa lake la Tanzania ili kupata mafanikio. " Eng. Kabeho.
Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyang'hwale, Katibu Tawala wa Wilaya, Ndugu Fabiani Yinza amewapongeza viongozi wa awamu zote za Uongozi hapa nchini kwa kuliletea taifa maendeleo.
"Bidhaa zetu zitashuka bei sana kutokana na uwepo wa reli ya kati na vijana wengi watapata ajira kupitia uwepo wa reli hii ya kati." Amesema.
Bi. Rhoda Simon, Mwalimu mstaafu aliyezaliwa tarehe 09 Desemba 1961 amemshukuru Mungu kwa uhai hadi anashuhudia nchi ikiadhimisha miaka 60 ya Uhuru na amesema miaka ya nyuma Geita mjini palikua na shule moja tu ya Sekondari ya wasichana lakini sasa shule za Sekondari ni nyingi jambo linalopelekea wanafunzi kutembea muda mfupi kufika shuleni.
Maadhimisho haya yameenda sambamba na Dua na Sala Maalum ya kuwaombea Viongozi na Taifa kuendelea kuwa na amani na kuwa Nchi yenye mafanikio na hatimaye liweze kukua kiuchumi siku hadi siku.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa