Na Boazi Mazigo-Geita
Benki ya NMB imeupongeza mkoa wa geita kufuatia ushirikiano na mahusiano mazuri ambayo ofisi ya mkuu wa mkoa imekuwa ikiutoa kwa taasisi hiyo ya kifedha katika utekelezaji wa majukumu yake mbalimbali ya kila siku, hali inayopelekea ufanisi mkubwa wa taasisi hiyo hadi kuiwezesha NMB kutoa kiasi kikubwa kama Gawiwo kwa Serikali
Hayo yameelezwa Julai 13 2022 na ujumbe kutoka benki ya NMB mbele ya Mkuu wa Mkoa Geita Mhe.Rosemary Senyamule walipomtembelea ofisini kwake kwa lengo la kushukuru na kumpongeza kwa ushirikiano wanaupata.
Akiongea kwaniaba ya ujumbe huo, Mkuu wa Taasisi za Serikali na Binafsi kutoka Benki ya NMB makao makuu Bw. William Makoresho amesema, " tunautambua mkoa wa geita kama mchangiaji mkubwa wa benki yetu na ndiyo maana hata gawiwo tulilolitoa la Bilioni 33 serikalini, Geita imechangia pakubwa, hongereni sana. Pia tuwapongeze kwa ushindi mkubwa wa timu ya geita gold kutoka Geita"
Bw.Makoresho ameongeza kuwa, NMB wanatarajia kuanza kuboresha ofisi zao za Geita kama ambavyo mkuu huyo wa mkoa amekuwa akiwashauri na kwamba wateja wategemee mabadiliko makubwa yenye maboresho zaidi huku wakieleza neema waliyoanza kuitoa kwa wachimbaji upande wa uwezeshwaji "mikopo ya dhahabu" ili wafanye shughuli zao kisasa na kwamba wataendelea kufanya kazi na serikali kwa kuchangia maendeleo lakini pia kutimiza wajibu wao kwa jamii (CSR)
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Geita Mhe.Rosemary Senyamule amesema "kama mkoa ninaipongeza benki yenu kwa kazi nzuri na ushirikiano mnaotupa serikali ya mkoa na niwapongeze kwa mikopo mliyoanza kuitoa (Mikopo ya Dhahabu) na hii ndiyo Geita ya Dhahabu"
Mhe.Senyamule amewaeleza NMB kuwa, mkoa wa geita unacho kiwanda cha kusafisha dhahabu geita (Geita Gold Refinery) GGR, hivyo waone namna ya kushirikiana na mwekezaji wa kiwanda hicho ili kuwawezesha wachimbaji wasafishe dhahabu zao kiwandani hapo penye uwezo wa kusafisha kilo 600 za dhahabu kwa siku kwa viwango vya kimataifa.
Aidha Mhe.Senyamule amewapongeza kwa kuitikia mapendekezo ya uboreshaji huduma za benki hiyo ikiwemo jengo kisha kuwaalika kushiriki maonesho ya kitaifa ya madini yatakayofanyika mkoani Geita na kuona namna ya kuweka miundombinu ya kudumu kwenye eneo la maonesho EPZA Bombambili mjini Geita.
Mwisho, Mhe.Senyamule amewakaribisha Benki ya NMB kutumia fursa ya uwanja wa mpira unaojengwa Halmashauri ya mji Geita wa timu ya Geita Gold ili waweze kuwekeza kwenye Miundombinu mbalimbali kama hoteli na kumbi za mikutano kwani uwanja huo utakapokamilika utafungua fursa mbalimbali kiuchumi kwa mkoa na taifa kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa