Waziri wa Madini Mhe.Dkt.Doto Biteko (Mb) ameshuhudia dhahabu iliyosafishwa kwenye kiwanda cha usafishaji wa madini hayo Geita Gold Reffinery (GGR) kilichopo mkoani wilaya na mkoa wa Geita kisha kumpongeza mwekezaji wa kiwanda hicho huku akiwasihi wachimbaji wadogo kupeleka dhahabu halisi kwenye kiwanda hicho.
Hayo yamejili Julai 7,2022 wakati waziri Dkt.Biteko alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Geita kwa lengo la kutembelea na kujionea namna kiwanda hicho kinavyofanya kazi akisisitiza umuhimu wa dhahabu inayochimbwa Tanzania kusafishwa hapa hapa nchini kisha akaipongeza GGR kwa namna ilivyoliheshimisha taifa.
“niwapongeze sana GGR kwa kuanza kazi, na kwa hali hii, mmelivisha nguo taifa kwani awali tulikuwa ni nchi ya kupeleka malighafi kwa wengine lakini kutokana na uwepo wa kiwanda hiki na hata Kongo watakuja. Niwahamasishe watanzania na wachimbaji mlete dhahabu zenu halisi hapa na ninaamini hakuna kukopwa ni kulipwa moja kwa moja” amesema Waziri Dkt.Biteko.
Ameendelea kuongeza kuwa, “Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anapenda kuona tunauza bidhaa zetu nje na si malighafi na ndiyo maana alishusha mrabaha kutoka 6% hadi 4% ili watu walete dhahabu yao isafishwe hapa nchini. Hivyobasi, uwepo wa shughuli hii unaongeza ajira, mapato ya serikali pamoja na maendeleo kwenye maeneo yetu”
Waziri Dkt.Biteko amemaliza kwa kuwapongeza mkurugenzi wa GGR Bi.Sarah Masasi kwa uthubutu licha ya kukatishwa tama pamoja na serikali ya mkoa kwa ushirikiano na namna inavyosimamia fedha za miradi hadi matokeo yake na akawaasa viongozi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji na kwamba kwa uwepo wa dhahabu ya akiba nchini utapelekea kuimarisha thamani ya fedha ya nchi.
Naye mkurugenzi wa kiwanda hicho Bi. Sarah Masasi amemhakikishia waziri wa madini kuwa wapo tayari kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu na kwamba kiwanda hicho husafisha dhahabu kwa viwango vya kimataifa “London Bullion” kwa 99.99% na kwamba kina uwezo wa kusafiisha kilo 600 kwa siku hiyvo, wachimbaji na wauzaji wa ndani na nje ya nchi wanakaribishwa.
Akiwasilisha salamu za mkoa, Mhe.Said Nkumba kwaniaba ya mkuu wa mkoa wa Geita amesema anamshukuru Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ndiyo maana Geita imeipata GGR hivyo kuamini kuwa matarajio ya mkoa yatafikiwa kwa uwekezaji unaonendelea na kwamba serikali mkoani hapa itaendelea kutoa ushirikiano na ulinzi na usalama utaendelea kuimarishwa hata nje ya eneo la kiwanda.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita Alhaj Said Kalidushi kwa upande wake amesema, “kwaniaba ya CCM, ile Geita ya dhahabu, utajiri na heshima sasa ndiyo imedhihirika sasa na mkoa huu utatangazwa kimataifa” hivyo kuwaomba wote kumuombea mwekezaji huyo asife moyo aendelee kusonga mbele kisha kumshukuru Mhe.Rais kwa kuwezesha wawekezaji wa ndani kuwekeza akimaliza kwa kusema “Mama Masasi umetuheshimisha Geita na nchi nzima kwa ujumla”
GEITA YA DHAHABU, UTAJIRI NA HESHIMA
Boazi Mazigo
Ag.HGCU
Geita RS
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa