Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Geita kwa namna ambavyo amekua mstari wa mbele kuhakikisha Askari Polisi ndani ya Mkoa wanapata makazi bora ya kuishi, huku akimuomba kufikisha ujumbe kwa viongozi wa dini ili kusaidia kukemea vitendo vya kiuharifu kama vile mauaji ya vikongwe na ubakaji kwani wao pia wana mchango mkubwa kwenye jamii katika kuhamasisha matendo yaliyo mema.
Ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazunguzo na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel tarehe 25.10.2018 akiwa katika ziara yake ya kikazi Mkoani Geita.
Amesema, “kwanza nakupogeza kwa kuteuliwa kuwa kiongozi wa mkoa huu, lakini pia kwa namna ambayo umekuwa ukihamasisha ujenzi wa nyumba za Askari kwa kushirikiana na RPC kwakuwa spidi ni kubwa sana na mkoa wenu ni wa nne sasa kutekeleza programu hii ya ujenzi ya “Self Help Scheme” inayosisitizwa na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Rais. Vilevile naomba viongozi wa dini watusaidie kupaza sauti juu ya vitendo viovu ikiwemo vya mauaji ya vikongwe na ubakaji”, kisha kuendelea na ziara yake.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Gabriel amempongeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Mwandamizi Msaidizi wa Polisi Mponjoli L.M mbele ya IGP Sirro akieleza namna ambavyo wanafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha kuwa amani na usalama vinatawala ndani ya Mkoa wa Geita vile vile akilishukuru Jeshi la Polisi Mkoa kwa ujumla kupitia utendaji wa askari ndani ya mkoa.
Mhandisi Gabriel ameongeza kusema, “tumekaa kama Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na tumesema hatukubali kuona Askari wanalala kwenye nyumba zisizo na heshima, bali walale mahali pazuri. Hivyo tulianzisha kampeni ya kujenga nyumba za askari mia moja (100) Kata ya Bombambili Mtaa wa Magogo Mjini Geita na tutapambana kuhakikisha fedha zinapatikana ili nyumba hizo zikamilike wahamie ili wanaoulinda uchumi wa Geita wafanane nao”
Awali Kamanda Mponjoli alieleza kuwa hadi sasa katika kampeni hiyo ya ujenzi wa nyumba 100, tayari kuna maboma tisa (9) ya mbili kwa moja (two in one) yaani nyumba kumi na nane (18), ambapo maboma hayo yapo katika hatua tofauti tofauti.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa