Katika kuhitimisha kilele cha wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama duniani ambayo kitaifa ilizinduliwa Agosti Mosi na kwa Mkoa wa Geita agosti 2, 2019 Mamlaka ya Mji Mdogo Katoro ndani ya Halmshauri ya Wilaya ya Geita, imesisitizwa kuwa, bado jamii inahitaji taarifa sahihi ili kuwasaidia wanawake wote waweze kunyonyesha na kutunza watoto wetu hatimaye tupate taifa lenye watu bora zaidi.
Msisitizo huo umetolewa agosti 7,2019 na Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Geita Dkt. Michael Mashala wakati akiahirisha wiki hiyo, huku akisisitiza juu ya kuongeza juhudi katika kuhakikisha utapiamlo unakomeshwa mkoani hapa na kuzipongeza redio za Rubondo Fm 105.3 na Strom Fm 88.9, redio za jamii zilizopo mkoani Geita kwa kutoa elimu ya unyonyeshaji maziwa ya mama.
“kwanza niwashukuru na kuwapongeza wadau USAID Boresha Afya kwa kushirikiana na IMA World Health pamoja na Amref Health Africa kwa kufanikisha wiki hii. Takwimu za unyonyeshaji wa maziwa ya mama zinaonesha tuko chini sana kwani ni asilimia 72.1 pekee ya watoto chini ya miezi 6 hunyonyeshwa, na asilimia 40.7 wakiendelea kunyonyeshwa maziwa ya mama mpaka wanapofikisha umri wa miezi 24”, alisema Dkt.Mashala.
Dkt.Mashala ameendelea kusema, unyonyeshaji wa maziwa ya mama unakabiliwa na changamoto za kukosekana msaada kwa mama/mzazi anayenyonyesha katika mazingira ya kazi, hivyo inahitaji kuwa na ushirikiano, taarifa zenye ushahidi na kuwasaidia akina mama na wazazi ili kuweka mazingira wezeshi ambayo humpa nguvu za kunyonyesha ipsavyo.
Aidha Dkt. Mashala amepongeza hatua ya utoaji wa elimu ya makundi ya vyakula na namna ya kuandaa na kuhifadhi vyakula hivyo, elimu ya unyonyeshaji kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ya uzazi na mtoto (RCH), kupima hali ya lishe kwa watoto wenye umri wa kuanzia miezi 0 hadi 59, ambapo jumla ya watoto 437 walipimwa na 7 kati yao kugundulika kuwa na utapia mlo mkali, watoto 21 kuwa na ule wa kadri(waliopimwa kituo cha kutolea huduma za afya Katoro na Masumbwe Mbogwe).
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi USAID Boresha Afya Dkt.Fredrick Venance ameshukuru ushirikiano wanaupata kutoka serikalini na kwamba huu ni mwaka wa kwanza wao kushiriki kwenye wiki hii ya unyonyeshaji na wana ahidi wataendelea kushiriki zaidi na zaidi.
Mwakilishi wa IMA World Health Bi.Gaudencia Gibai ameendelea kuwakumbusha akina mama kuwanyonyesha watoto na si akina baba ili kupata mtoto mwerevu na kusema wataendelea kushirikiana kufadhili maadhimisho kama haya mwakani kwakuwa hufanya kazi hiyo kwa kushirikiana na wadau wenza USAID Boresha Afya na Amref Africa.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bw.January Bikuba amewashukuru wadau hao akiwaambia kuwa, kama halmashauri wanatambua na kuthamini mchango wanaoutoa kwenye jamii katika kuboresha afya ya wananchi na kuwaasa waliohudhuria wiki hiyo kutumia yale yote waliyoelekezwa huku akiwapongeza wanaume waliohudhuria kilele cha wiki hiyo.
Mganga Mkuu Halmashauri ya Wilaya ya Geita Dkt. Deo Kisaka amewakumbusha akina mama waliohudhuria kuwafikishia elimu wengine ambao hawakufanikiwa kuipata.
Bi Vumilia John kwaniaba ya akinamama wa Katoro ameahidi kuwa balozi kwa wanawake kuwanyonyesha watoto maziwa ya mama pekee kwa umri wa 0 hadi miezi 6 ili kuwa na mtoto mwerevu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa