Na Boazi Mazigo - Geita
Ili kutimiza adhma ya serikali kuandaa wataalam wabunifu wa kizazi kinachokuja, mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe.Rosemary Senyamule amewataka wote wanaodhani Lishe suala la hiari kuacha mara moja na watekeleze kama ilivyo maelekezo na malengo ya serikali kuwa na jamii yenye lishe bora.
Hayo yameelezwa wakati mkuu wa mkoa huyo akiahirisha kikao mkakati kilichoketi katika Julai 13, 2022 katika ukumbi wa Nyerere EPZA Bombambili kilichofanyika kujadili agenda mbalimbali ikiwemo ufanikishaji mapokezi ya mbio za mwenge wa uhuru ,zoezi la sensa ya watu na makazi, utambuzi wa mifugo pamoja na masuala ya Lishe ndani ya mkoa wa Geita.
Mhe.Senyamule Amesema, " mkoa wa geita haujafanya vizuri kwenye suala la lishe kwa mwaka uliopita kutokana na baadhi ya watendaji na watumishi kutokutilia maanani suala la lishe. Lishe si hiari ni lazima kama ilivyoelekezwa na Serikali kwani serikali imeweka programu hii kuwa kila Halmashauri itenge shillingi 1,000 kwa kila mtoto lengo ni kuandaa wataalam na wabunifu wa kesho wa taifa hili"
Ameongeza kuwa, Viongozi ni muhimu kuwa mfano kwa jamii hata kwa kuwa na vitalu vya mbogamboga ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha lishe bora kwa jamii.
Vilevile, Mhe.Senyamule ameeleza juu ya viongozi kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi kushiriki mbio za mwenge wa uhuru na kuhakikisha miradi yote itakayopitiwa na mbio hizo kuanzia tarehe ya 20 Julai, 2022, iwe imeandaliwa vizuri bila kukosekana kwa taarifa na viambatisho muhimu na kwamba kwa watakaokwamisha upatikanaji wa nyaraka za miradi hiyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa na serikali.
Ameongeza kuwa, kwa sasa lipo zoezi linaloendelea la utambuzi wa mifugo kwa kuweka alama (hereni) ambapo bado zoezi hilo liko nyuma kiutekelezaji hivyo kutoa msisitizo wa kuendelea kuwahamasisha wananchi wafugaji kushiriki zoezi hilo muhimu la kupeleka mifugo waliyonayo kwa utambuzi kulingana na maeneo yaliyowekwa kwa kila Halmashauri.
Aidha, Mhe.Senyamule amezipongeza TRA na Halmashauri zote za mkoa wa Geita kwa kufanikisha ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2021/2022, lakini pia pongezi zimeelekezwa kwenye halmashauri kwa kufanikisha kwa kiasi kikubwa zoezi la anwani za makazi.
Mwisho, Mhe.Senyamule ametoa pongezi kwa vyama vya siasa rafiki (ambavyo vilizoeleka kwa jina la vyama vya upinzani) kwa ushiriki wao akiwakaribisha kuendelea kushiriki hata wakati wa mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka 2022.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa