MAADHIMISHO YA SIKU YA CHAKULA DUNIANI KITAIFA YAZINDULIWA MKOANI GEITA
Siku ya Chakula Duniani uadhimishwa kila tarehe 16 ya Mwezi Oktoba na nchi zote ambazo ni mwanachama wa Shirika la Chakula Duniani.Nchini Tanzania Kitaifa maadhimisho haya yamefanyika Mkoa wa Geita katika Uwanja wa CCM Kalangalala uliopo Halmashauri ya Mji Geita.
Akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho haya mgeni rasmi Mheshimiwa Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga Mkuu wa Mkoa wa Geita amewataka wananchi kuhudhuria katika mabanda mbalimbali ya maonyesho ili kupata elimu na kuona ubunifu unaotumiwa ili nao wakaongeze uzalishaji katika maeneo yao. "Ni mategemeo yangu kuwa wote mliofika hapa mtapata fursa ya kuangalia na kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanywa na wakulima, wavuvi, wafugaji, wafanyabiashara, wajasiliamali na taasisi mbalimbali za umma na binafsi katika kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa na usalama wa chakula na kuboresha uendelezaji wa sekta ya kilimo".
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi kuacha tabia ya kuharibu misitu kwa kukata miti hovyo, kulima katika hifadhi kwa kuwa vyote hivi vina athari kubwa kwa mazingira hivyo kupelekea upungufu wa Chakula kutokana na uhaba wa mvua.
Lengo la kuwa na maadhimisho haya ni kuhamasisha jamii kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula kwa tija ili kuwa na mavuno mengi yanayokidhi mahitaji ya wakazi wa Geita, Tanzania na Dunia kwa ujumla. Kaulimbinu ya maadhimisho kwa mwaka huu inasema ‘‘Badili mwelekeo wa uhamaji: Wekeza kwenye Usalama wa Chakula na Maendeleo Vijijini’’.
Maadhimisho haya yanatoa fursa ya kutambua mchango muhimu unaotolewa na wakulima wadogo wadogo, jamii za wavuvi na wafugaji katika maendeleo endelevu na katika kutimiza mkakati wa kutokomeza njaa kupitia mifumo endelevu ya chakula. Maadhimisho haya yanaangazia sehemu tatu za uendelevu, ambazo ni kiuchumi, kijamii na kimazingira, ikumbukwe kuwa mashamba ya kaya huleta pamoja sehemu zote tatu na kubwa zaidi ni kuhakikisha kunakuwepo na maendeleo ya kiuchumi na uhakika wa chakula.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa