Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Ndugu Mohamed Gombati ametoa maelekezo kwa Maafisa Maendeleo ya jamii wanaofanya kazi katika Mkoa wa Geita kuhakikisha wanakuwa daraja litakalowavusha wananchi kiuchumi kutoka hatua moja hadi nyingine.
Ndg. Gombati ametoa kauli hiyo hivi karibuni alipokuwa akifungua rasmi kongamano la kwanza la Maafisa Maendeleo ya jamii Mkoa wa Geita lililofanyika katika ukumbi wa Nyerere uliopo kwenye viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Geita mjini hivi karibuni.
Katibu Tawala Mkoa wa Geita amefafanua kuwa moja ya jukumu la Maafisa Maendeleo ya jamii ni kutambua fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana katika maeneo yao zikiwemo za kilimo cha umwagiliaji, ufugaji, biashara ndogondogo na nyinginezo.
“Jamii yoyote iliyo bora inajengwa na Maafisa Maendeleo ya jamii hivyo hakikisheni fursa zote zilizoko katika maeneo yenu zinachangamkiwa na kutumiwa ipasavyo, ikiwemo fursa ya mikopo yenye riba nafuu inayotolewa na Serikali pamoja na taasisi nyingine za kifedha sambamba na ruzuku nyinginezo kama vile pembejeo za kilimo, mifugo nk.” Aliongeza Ndg. Gombati.
Afisa Maendeleo ya jamii Mkoa wa Geita Bi. Martha Kaloso ameeleza kuwa lengo kuu la kongamano hilo ni kujenga uelewa wa pamoja katika kusimamia taratibu kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kujenga jamii kwa ufanisi mkubwa na anaamini kuwa kongamano hilo litaongeza uwajibikaji kwa jamii kupitia Maafisa Maendeleo ya jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Maafisa Maendeleo ya jamii wenzake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale Bw. Majagi Maiga ametoa shukrani kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kutambua umuhimu wa Maafisa Maendeleo ya jamii wa Mkoa mzima kukutanishwa ili kujadili changamoto zinazowakabili katika maeneo yao, kubadilishana uzoefu wa kazi na kuweka mikakati ya namna ya kujikwamua kutoka katika changamoto zinazowakabili katika utendaji kazi wao wa kila siku.
Kwa upande wake mwezeshaji Carlos Gwamagobe kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum amewataka Maafisa Maendeleo ya jamii katika Mkoa wa Geita kuendelea kuwasaidia wananchi kuchangamkia fursa nyinginezo za kiuchumi na siyo kutegemea shughuli za uchimbaji madini pekee.
Kongamano la kwanza la Maafisa Maendeleo ya Jamii katika Mkoa wa Geita liliongozwa na Kauli Mbiu isemayo “ Uchechemuzi ni dira ya matokeo chanya kwa jamii” moja ya shughuli iliyofanyika ndani ya kongamano hilo ni utoaji tuzo kwa Maafisa Maendeleo ya jamii waliofanya vizuri katika kuhamasisha wanufaika kurejesha mikopo inayotolewa na Serikali kwa vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum ndani ya muda unaotakiwa ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Chato imeibuka kinara ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe na Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale imeshika nafasi ya tatu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa