Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalum Bw. Amon Mpanju amewaasa Maafisa Maendeleo ya Jamii waliopatiwa pikipiki ambazo zimetolewa na Serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuzitunza pikipiki hizo na kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na sio shughuli zao binafsi.
Bw. Mpanju ametoa wito huo tarehe 24 Oktoba 2024 alipokuwa akikabidhi pikipiki nane kwa Maafisa Maendeleo ya jamii wa Kata za Muganza, Kigongo, Lwamgasa, Shabaka, Uyovu, Namonge, Masumbwe na Lulembela. Hafla fupi ya ugawaji wa pikipiki hizo umefanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejikita katika kutekeleza matakwa ya kikatiba ya kugatua rasilimali fedha, ushushaji wa huduma Pamoja na watumishi ili kuwafikia wananchi wote walioko katika vitongoji, vijiji, mitaa na Kata na katika hili ndani ya miaka miwili Sekta ya Maendeleo ya Jamii imeajiri watumishi zaidi ya elfu moja.

“Serikali imeona kuajiri wataalam wa Maendeleo ya Jamii kwenye Kata pekee bila kuwapatia vitendea kazi inakuwa haitoshi kama tunavyojua jiografia ya Nchi yetu ni pana, kuna baadhi ya wananchi wanaishi mbali na Makao makuu ya Halmashauri. Hivyo Maafisa Maendeleo ya Jamii ambao ni wachechemzi na wahamasishaji wakubwa wa maendeleo ambao wanatakiwa wahakikishe wananchi wanatambua fursa mbalimbali zinatozolewa na Serikali ikiwemo mikopo yenye riba nafuu kwa kuwahamasisha katika maeneo yao.
Bw. Mpanju ameongeza kuwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata wana uwezo, mbinu na kuamsha ari ya maendeleo katika ngazi ya msingi kwa kutekeleza majukumu mbalimbali kwa manufaa ya jamii lakini wanahitaji nyenzo za kuwawezesha kuwafikia wananchi hao. Hivyo katika kutambua hilo Serikali imeweka utaratibu wa kununua pikipiki kila mwaka, ambapo katika mwaka wa fedha 2025/2026 imenunua pikipiki 98 kwa Nchi nzima ili kuboresha utendaji kazi wa Maafisa hao wakishirikiana na wataalam wengine kwenye Kata na kutimiza majukumu yao kiufanisi.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Geita Bi. Martha Kaloso ameeleza kuwa Idara ya Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Geita inakabiliwa na uhaba wa vyombo 131 vya usafiri kwa wataalam wake katika ngazi ya Kata hali inayopelekea uwajibikaji hafifu wa kuwafikia wananchi walioko maeneo ya vijiji vya mabli, ufuatiliaji hafifu wa shughuli za miradi ya maendeleo ya Jamii na ufuatiliaji hafifu wa mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Ndg. Wajama Bwire, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Namonge Wilaya ya Bukombe ametoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwakumbuka na kuwapatia pikipiki zitakazowawezesha kutoa huduma kwa wananchi katika maeneo ambayo yako mbali na makao makuu ya Halmashauri zao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa