MAWAZIRI UGANDA WAVUTIWA NA UCHIMBAJI MDOGO WA DHAHABU MKOANI GEITA
Mawaziri wa nne wa Wizara za Madini, Uchumi, Mambo ya Ndani na Nje wa Serikali ya Jamhuri ya Uganda wamewasili Mkoani Geita kujifunza namna Serikali ya Tanzania ilivyofanikiwa kuwezesha na kuendeleza Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu ili kukuza Sekta hiyo nchini kwao.
Akizungumza kwa niaba ya Mawaziri wengine baada ya kuwasili katika Mgodi wa Busolwa Mine Waziri wa Nchi na Maendeleo ya Madini wa Uganda Mheshimiwa Lokeris Peter amesema kuwa wamekuja Tanzania kujifunza mbinu za kuendeleza Sekta ya Madini hususan Uchimbaji Mdogo kwa kuwa Tanzania imekuwa ikifanya shughuli hii kwa muda mrefu na kupata mafanikio makubwa. Mheshimiwa Peter ameongeza kuwa wamekuja Geita kwa kuwa ni kuna migodi mingi mikubwa na midogo hivyo wamekuja kujifunza namna wanavyochimba, kuuza, kuunganisha wachimbaji katika vikundi na namna wanavyothibiti utoroshaji wa madini ili nao wakawaendeleze wachimbaji wa dogo nchini Uganda kwa nia ya kupata maendeleo kama Tanzania.
Awali akizungumza katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Stanslaus Nyongo Naibu Waziri wa Madini amesema kuwa Tanzania tumepata maendeleo makubwa ya kuweza kuendeleza wachimbaji wadogo, kati na wakubwa hivyo Mawaziri wanne na Wanasheria kutoka Uganda wamekuja nchini kuona ni jinsi gani Serikali ya Tanzania ilivyofanikiwa kuendeleza na kusaidia uchimbaji wa madini mdogo, kati na mkubwa. Amesema "wametembelea nchi nyingine za Afrika lakini bado wameona kuna umuhimu wa kufika Tanzania kwasababu kila nchi waliyofika waliona Tanzania ni mfano kwa Afrika hivyo wamekuja kujifunza na kuona namna nchi inavyoneemesha wananchi wake kupitia sekta ya madini baada ya mabadiliko ya sheria ya madini ya mwaka 2010 kwenda Sheria mpya ya mwaka 2017 na mabadiliko yake na sera za nchi kwa jumla ". Ameongeza kuwa wamekuja Geita kwasababu kuna madini na wachimbaji wadogo wengi zaidi ili waone jinsi wachimbaji wadogo wanavyowezeshwa kupata mitaji ya kufanya shughuli za uchimbaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ameipongeza Serikali ya Uganda kwa kuona umuhimu wa kuja kujifunza Geita na kutambua jinsi Sekta ya madini inavyoweza kuleta mageuzi ya uchumi wa nchi. Ametoa wito kwa wachimbaji wadogo mkoani hapa kujiunga katika vikundi ili kuunganisha nguvu, mitaji na uzoefu wao kwa pamoja na walete vifaa vya kisasa na kuwa na uchimbaji wa kisasa wenye tija ili mitaji yao ipanuke na kupata faida ili kuongeza ajira nyingi kwa watanzania.
Wakiwa Mkoani Geita Mwaziri hao pamoja na wataalamu wao wametembelea Wilaya ya Geita ambapo wamejionea shughuli za uchimbaji mdogo na kati katika migodi ya Busolwa mine uliopo kata ya Nyarugusu,Kadeo Mine na Kituo cha mfano cha Serikali kwa ajili ya kufundishia masuala ya uchimbaji wa madini kilichopo eneo la Lwamgasa Wilayani Geita.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa