Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amefungua soko moja la madini ya dhahabu Mjini Masumbwe Wilayani Mbogwe, soko linalofanya mkoa huu kuwa na idadi ya masoko kuwa matano ndani mkoani geita agosti mosi, 2019 huku akiwakumbusha wanachi kuendelea kuwaombea vingozi wakuu wa nchi kwa yale yanayoendelea kufanyika.
Akizungumza baada ya kufungua soko hilo, Mhandisi Gabriel ameipongeza mbogwe kuwa wilaya ya pili kuanzisha soko la madini huku akiwataka wafanyabaishara wanaojihusisha na dhahabu kuhakikisha dhahabu haitoroshwi na inafika sokoni hapo ili serikali iweze kupata mapato na kuonya viongozi wanaoshiriki kuleta dhuluma kwenye shughuli za uchimbaji dhahabu na kusema soko hilo liwe chichu ya masoko wilaya nyongine za mkoa wa geita.
Amesema, “nawapongeza sana kwa uanzishaji wa soko la dhahabu. Soko hili limeweka historia kubwa kutokana na kwamba taarifa ya mwezi wa saba mwaka huu pekee inaonesha tumepata kilo 305 za dhahabu sawa na asilimia 200 ukilinganisha na mwaka 2018 kipindi kama hiki. Mpaka sasa, Geita tunaongoza kwa uzalishaji wa dhahabu kwa kuwa na asilimia 48 hadi 50”
Mhandisi Gabriel ameendelea kusema, mwezi aprili mwaka 2018 kufuatia utoroshwaji wa kaboni, mkoa uliweza kukusanya kilo 88 kwa huo mwezi, lakini baada ya zuio la kusafirisha kaboni, miezi iliyofuata kulikuwa na ongezeko ambapo zilipatikana kilo 135, kisha, 145, 152, na 175. Lakini baada ya kuanzishwa kwa soko kuu la dhahabu geita lililofunguliwa mwezi aprili, 2019 na waziri mkuu mhe. Kassim Majaliwa, mkoa ulipata kilo 200 za dhahabu, kisha mwezi wa tano kilo 196, wa sita 194, na wa saba kilo 305, hatua inayostahili pongezi kubwa mno.
Lakini pamoja na kupatikana kwa kilo hizo, bado mhandisi Gabriel anasema ipo haja ya kuongeza juhudi na kufikisha hadi kilo 145 pamoja na lengo la mkoa kwenye mapato ya dhahabu la kukusanya Bilioni 156 kwa mwaka 2019/20 akiamini kuwa ndani ya kipindi kifupi mkoa utakua na masoko 9 katika maeneo mbalimbali yenye shughuli za uchimbaji wa dhahabu ambapo kwa sasa masoko yaliyopo ni soko kuu la dhahabu geita na masoko madogo ya Katoro, Nyarugusu, Nyakagwe na Mbogwe.
Maonyo yakatotolewa kwa viongozi wenye uwezo na madaraka wanaotumia vibaya nafasi zao na kusababisha dhuluma kwa wachimbaji huku wavamizi wa maeneo ya uchimbaji kutakiwa kusubiri utaratibu maalum na si kuvamia maeneo hayo ukizingatia serikali ya awamu ya tano kupitia wizara ya madini tayari imefuta leseni nyingi zilizokuwa hazifanyiwi kazi.
Akisoma taarifa ya soko kwaniaba ya mwenyekiti wa soko la dhahabu mbogwe, Bw. Bunga Dadu Gakola amesema, uanzishaji wa soko hilo ni utekelezaji wa maagizo kwa wafanyabiashara na wachimbaji wadogo wa dhahabu kutouza dhahabu yao kiholela na kuikosesha serikali mapato na badala yake kuwa na sehemu moja ili kurahisisha ulipaji wa mapato ya serikali na kuiweka sekta ya madini hasa wachimbaji wadogo katika hali nzuri ya kiuchumi (hizi ni faida) kwakuwa tayari Mhe.Rais Magufuli amekwisha kuounguza kodi ambazo zilichangia wengi kutorosha madini hayo.
Bw. Gakola ameendelea kusema kuwa, kwa sasa soko hilo lina jumla ya wafanyabiashara wadogo wa dhahabu 6 wenye majiko ya kuchomea dhahabu na kwamba uongozi unaendelea kuwakaribisha wafanyabiashara wengine kwakuwa vyumba bado vipo.
Ombi la wafanyabiashara hao likawa ni uimarishwaji wa ulinzi na usalama katika jengo hilo ili kuwawezesha kufanya biashara kwa usalama wa mali zao ikiwa gharama za matengenezo ya jengo hilo pamoja na kukodishwa ni zaidi ya shilingi mil 37
Bw. Ernest Kafu Maganga ambaye ni kaimu afisa madini mkazi mkoa wa geita amesema, wilaya ya mbogwe ina jumla ya leseni za utafiti 46, leseni 1 ya uchimbaji wa kati, leseni za uchimbaji mdogo wa madini 87, miradi ya uchenjuaji wa madini ya dhahabu 40 zikiwemo elutions na leseni 6 ndogo za biashara ya madini.
Bw.Kafu ameendelea kusema, mwaka 2017 yalifanyika marekebisho ya sheria ya madini ya mwaka 2010 kupitia marekebisho Na.7/2017 kama jitihada za serikali kudhibiti utoroshwaji madini nchini ambapo kifungu cha 27C (1 na 2) cha Marekebisho ya Sheria hiyo kinaelekeza kuanzishwa kwa masoko ya madini kama ambavyo mbogwe wamefanya na kwamba kupitia hatua hii, kumekuwa na ongezeko la vibali vya usafirishaji wa madini nje ya nchi, ongezeko la wafanyabiashara wakubwa wa madini kutoka wafanyabiashara 3 hadi 10 kwa soko kuu la madini geita bila kusahau udhibiti utoroshwaji na uuzwaji madini kinyemela.
Kwa upande wa viongozi wa CCM Wilaya ya Mbogwe, wameendelea kupongeza juhudi na hamasa iliyoanzishwa na mkuu wa mko wa geita na kwamba huo ni utekelezaji wa ilani wa hakika.
Hafla hiyo pia imehudhuliwa na mbunge wa jimbo hilio Agostino Nyanda Maselle, baadhi ya wajumbe wa KUU wilaya, wafanyabiashara wa madini ya dhahabu, watumishi kutoka sekretariet ya mkoa na wataalam wa halamshauri bila kusahau viongozi wa CCM Wilaya na wananchi wa Mbogwe.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa