Mkuu wa Mkoa Geita Mhe.Martine Shigela amekemea tabia ya baadhi ya watendaji wa serikali mkoani hapa kuchelea kutekeleza maagizo ya viongozi hususan wale wa Kitaifa kisha kuipongeza Halmashauri ya Wilaya Mbogwe kwa ufanisi katika kutekeleza afua zote za Lishe kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Alieleza hayo wakati akifungua kikao cha Lishe cha robo ya nne kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kilichofanyika Julai 20, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa na kuwataka watendaji kuwajibika ipasavyo na kutekeleza maagizo ya viongozi bila kusita.
“Suala la Lishe ni kipaumbele cha Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, ni muhimu sana na ndiyo maana kila mikutano ninayoifanya nimekuwa nikiwakumbusha, hivyo niwapongeze Mbogwe kwa kutekeleza vizuri Afua zote za lishe na kupata alama nzuri”, alisema RC Shigela.
Aliongeza kuwa, “ni vyema watendaji nanyi mtambue maagizo ya kiongozi wetu mkuu wa kitaifa hayajadiliwi, ni utekelezaji tu, hivyo kwakuwa tunaanza mwaka mpya, nendeni mkatekeleze”.
Kwa upande wake Katibu tawala mkoa Geita Prof.Godius Kahyarara alisema, miongoni mwa malengo ya kikao hicho ni kukumbushana jukumu kubwa ambalo mkoa ulikabidhiwa na Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan la kusimamia masuala ya lishe kupitia mkataba uliosainiwa, hivyo kila mmoja atambue vyema majukumu yake na kwamba kikao hicho kitumike kujitathmini na kutoa mawazo mapya ya namna ya kutekeleza afua za lishe kwa ukamilifu.
Awali akitoa taarifa ya hali ya utekelezaji, mganga mkuu mkoa geita Dkt.Omari Sukari alianza kwa kumpongeza RC Shigela kufuatia usimamizi na ufuatiliaji mzuri wa afua za lishe kama ilivyoainishwa kwenye mkataba. Pia alisema, “pamoja na kufanya vizuri kwenye viashiria vyote, changamoto ilikuwa upande wa utoaji wa fedha. Hivyo udumavu katika ngazi ya mkoa ilikuwa 38.6%, ukondefu 3.3%, uzito pungufu 10.2% na upungufu wa damu kwa wajawazito nao walikuwapo kiasi”
Mwisho, wajumbe walisistizwa juu ya kusimamia utekelezaji wa maagizo ya viongozi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa