Na Boazi Mazigo-Geita
Ikiwa zimesalia siku kumi na mbili kufikia siku ya kupokea taarifa ya suluhu ya kudumu ya mgogoro uliodumu kwa muda mrefu baina ya Wananchi wilayani Geita na Mgodi wa Dhahabu Geita (GGML) kuhusu fidia kwenye eneo lenye leseni ya uchimbaji inayomilikiwa na mgodi huo, mkuu wa mkoa Geita mhe.Martine Shigela amefanya ziara na kujionea uhalisia mipaka iliyowekwa kwenye eneo llinalouzunguka mgodi huo na kuwaomba wananchi kuendelea kuwa na utulivu wakisubiri uamuzi wa serikali juu ya hatima yao.
Akiongea baada ya kutembelea maeneo kadha wa kadha yenye vigingi vya mipaka ya mgodi huo Desemba 28, 2022, RC Shigela amesema ameona ni vyema kutembelea maeneo hayo yenye mgogoro ili kumsaidia pamoja na viongozi wengine kufanya maamuzi sahihi pale hatua ya kufanya hivyo itakapofikiwa huku akiwaahidi wananchi kuwa serikali iliyopo madarakani inamaliza changamoto waliyonayo hivi karibuni.
“kwanza niwashukuru viongozi wote kuanzia serikali za Mitaa, wananchi pamoja na mgodi kwa kazi tuliyoifanya kwa kushirikiana. Ninaamini mgogoro wa shambani, humalizwa shambani na ndio maana nilionelea nifike kuona kwa macho ili hata tunapokuwa kwenye hatua za maamuzi ya kupata suluhu ya kudumu basi tufanye tukiwa tunayaelewa vyema maeneo haya” alisema RC Shigela.
Aidha mkuu wa mkoa huyo aliongeza kuwa, ziara hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi madhubuti wa Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan baada ya kikao na viongozi wa juu wa mgodi na kwamba imedhamiria kuumaliza kabisa mgogoro huo ndani ya kipindi kifupi ili kuwaondolea adha wananchi wa Geita ili waweze kujiletea maendeleo na kuwapongeza viongozi kuanzia mbunge, diwani hadi mwenyekiti wa mtaa kwa namna wanavyofuatilia utatuzi wa kero hiyo.
Kwa upande mwingine, mkurugenzi mtendaji wa mgodi huo Bw.Terry Strong amesema anaushukuru uongozi wa serikali kwa jitihada na amejifunza mengi na hasa kuhusu mgogoro huo na kwamba wanahidi suluhu itapatikana kwani kupitia changamoto ndipo huibuka namna ya kutatua.
Ziara hiyo imehusisha viongozi mbalimbali wa serikali, Chama Cha Mapinduzi, pamoja na wananchi ambapo maeneo mbalimbali yametembelewa ikiwemo eneo la Katoma, Magema, Katumaini, Nyamatagata, Mgusu, Nyakabale n.k
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa