Na Boaz Mazigo-Geita
Katika kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliotupatia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkoa wa Geita umeadhimisha sherehe za Muungano wilayani Nyang'hwale kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa miradi ya Maendeleo.
Akizungumza na wananchi pamoja na viongozi mbalimbali waliokusanyika Aprili 24,2023 katika uwanja wa Sabasaba, Mkuu wa Mkoa Geita Mhe.Martine Shigela amesema ni vyema kuendelea kumshkuru Mungu kuipatia Tanzania viongozi wenye hofu ambao wameweza kuudumisha Muungano jambo linalofanya taifa letu liendelee kuwa na umoja, mshikamano na maendeleo, huku akiipongeza Nyang'hwale kwa kuwa na shule ya serikali ya mchepuo wa kiingereza aliyoizindua kabla ya kuhutubia wananchi.
"Miaka 59 ya Muungano ni mafanikio yetu sote, taifa letu limeendelea kuwa la Amani na Mshikamano. Sisi ni Kabila Moja, Sisi ni Taifa moja. Tumepiga hatua kwenye elimu, afya, maji, barabara, n.k. Zamani kwenda shule kusoma ilikuwa kuchaguliwa lakini sasa tunashindana kwa vigezo, anayefaulu anaenda kusoma. Muungano umetufanya kuwa kitu kimoja na hii ni kutokana na misingi iliyowekwa, tuudumishe" alisema RC Shigela.
Awali akizindua shule ya msingi mchepuo wa kiingereza Kharumwa, iliyojengwa kutokana na fedha ya CSR ya zaidi ya Milioni 420 ya Mgodi wa Barrick, RC Shigela amesema ipo haja ya kuongeza wigo kwa wananfunzi kujiunga na shule hiyo akisema "shule hii itatukumbusha muungano. Niwapongeze wazazi kuleta watoto kwenye shule hiyo na tunataka kuwaona watoto wa Nyang'hwale wakitamba duniani. Tusijenge matabaka kwenye jamii na michango isiwe kigezo kukwamisha watoto kupata elimu".
RC Shigela alisema pia anaupongeza uongozi wa Nyang'hwale na kusema kuwa, Serikali chini ya Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan inandelea kutengeneza mazingira mazuri kwa wananchi wake, hivyo viongozi na wananchi waendelee kuinga mkono kisha kuwahimiza kupanda miti na kutunza mazingira lakini pia wananchi ni vyema wasivamie maeneo ya shule, yahifadhiwe ili yatumike kwa baadaye.
Mwisho alihitimisha kwa kutoa pongezi kwa mshindi wa Insha ya Muungano kwa Bi.Donatha Kamanzi Denis, kidato cha tano, Shule ya Sekondari Msalala
Naye Bi.Alexandrina Katabi kwaniaba ya Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa alisema ni vyema kuendelea kuudumisha Muungano na ni vyema wananchi kujiandaa vyema kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na ule mkuu pale utakapofika kwa amani na upendo ili kuendelea kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wao wakuu wa wilaya za Mbogwe Mhe.Sakina Mohamed na Chato Mhe.Deusdedith Katwale kwa nyakati tofauti wasema katika maeneo yao miti imepandwa na itaendelea kupandwa ili kutunza mazingira na wananchi wanaendelea na usafi wa mazingira huku wakihimiza kuulinda na kuudumisha Muungano
Miaka 59 ya Muungano, Umoja na Mshikamano Ndiyo Nguzo ya Kukuza Uchumi
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa