Serikali ya Awamu ya Tano Kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji Geita ipo mbioni kuanzisha kituo kimoja cha uimarishaji na uendelezaji biashara (one stop business formalization and development centre) katika jengo la soko kuu la dhahabu geita ikiwa ni miongoni mwa jitihada za serikali katika kuweka mazingira mazuri ya biashara kwa kuruhusu uwekezaji mkubwa wa kibiashara Mjini Geita.
Hayo yameelezwa Julai 4, 2019 Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Bw.Deodatus Kayango, akimwakilisha mkuu wa mkoa wa geita alipokuwa akisoma hotuba ya kuahirisha mafunzo ya siku 4 kwa washiriki 614 (wafanyabiashara na wajasiriamali) yaliyoandaliwa na MKURABITA katika ukumbi wa kanisa la Katoriki Mjini geita.
Akiahirisha mafunzo hayo, Bw.Kayango amesema kuwa, anaamini mafunzo yaliyotolewa yamewajengea uwezo wa kufanya biashara washiriki hao katika mfumo rasmi kwani kurasimisha biashara kutakuza biashara zao na kutawapa fursa kufanya kazi na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi kwa utaratibu wa zabuni, hivyo waichangamkie fursa kwakuwa Geita ni mkoa wa kimkakati.
“tambueni kuwa, uanzishwaji wa soko la madini na maandalizi ya eneo la uwekezaji kwaajili ya maonyesho ya biashara pamoja na shughuli za uchimbaji wa dhahabu utafungua fursa mbalimbali za uwekezaji, hivyo mzichangamkie fursa hizo kwani sasa mnaweza kuzibaini. Nawasihi kuwa makini kuyafanyia kazi mliyoyapata ili muweze kuboresha kipato muboreshe na maisha yenu lakini kubwa zaidi, tusichakachue bidhaa zetu”, amesema Kayango
Akihitimisha, Bw. Kayango amewakumbusha kujifunza uzalendo kwa kutoa na kudai risiti wakati wa biashara na pia anaamini mafunzo kutoka kwa wawezeshaji yatakuwa na tija kwao, kisha kukabidhi vyeti kwa baadhi ya washiriki.
Naye mwakilishi wa mkurugenzi wa mji geita bw. Zengo Pole ambaye ni Afisa Maendeleo ya Vijana amesema anawashukuru wawezeshaji wote pamoja na wadau MKURABITA kwa kuichagua geita. Vilevile amesema, kama halmashauri wako tayari kuwapokea wadau wengine wowote wa maendeleo na kuwashika mkono wafanyabiashara ili kuwakuza na ndiyo maana wanatoa asilimia 10 ya wanawake, vijana na wenye ulemavu na kuwashauri waitumie elimu waliyonayo wakichukua mikopo kutoka halmashauri ili wajiendeleze.
Awali akisoma taarifa fupi ya utangulizi mbele ya mgeni rasmi, meneja urasimishaji biashara wa MKURABITA bw. Harvery Kombe amesema, mafunzo hayo yalilenga kuwafikia watu 1000 lakini wameweza kutoa kwa 617 pekee. Vilevile wawezeshaji wametoka MKURABITA, benki na NMB, CRDB, TCCIA, SIDO, GODTEC, NSSF, STAMICO na halmashauri.
Uwepo wa Kituo cha urasimishaji na uendelezaji biashara utahusisha kupata kitambulisho cha uraia kutoka NIDA, kusajili majina ya biashara (BRELA) kutoa leseni za biashara, namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN) kupitia TRA, huduma za kibenki kutoka CRDB na NMB, na TBS kupitia SIDO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa