MKUU WA MKOA ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA LIPA KWA MATOKEO HALMASHAURI YA MJI GEITA
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel imeipongeza Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kusimamia vizuri fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa vilivyo chini ya mpango wa lipa kwa matokeo shule ya msingi Nguzo mbili.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika shule hiyo Mheshimiwa Robert Gabriel amesema kuwa ameridhishwa na kiasi cha fedha kilichotumika katika ujenzi wa madarasa kwa ubora wa hali ya juu katika shule hiyo. " Inashangaza sana kuona maeneo mengine wanatumia fedha zote kiasi cha shilingi 20 milioni katika ujenzi wa darasa moja lakini kuna mapungufu mengi hivyo lazima kuwe na nidhamu ya matumizi ya fedha katika miradi ya Serikali".
Shule ya Msingi Nguzo mbili imejenga madarasa nane kwa kutumia shilingi milioni 13 kwa kila darasa, Ofisi 4, kisima cha maji na vyoo vya kisasa pamoja na ukarabati wa madarasa mengine katika shule hiyo kutokana na fedha iliyobaki katika bajeti ya darasa moja.
Akiwa shuleni hapo Mkuu wa Mkoa ameagiza wakurugenzi kuunda na kutumia vikundi vya ujenzi vilivyo katika maeneo ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa madarasa pia kuishirikisha jamii ili kupunguza gharama kwa serikali na hatimaye fedha zinazobaki ziwezekufanya mambo mengine katika huduma za jamii.
Katika hatua nyingine Mhandisi Robert Gabriel ameutaka uongozi wa Shule ya Msingi Nguzo Mbili kusimamia suala la usafi na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita kuhakikisha anasimamia uimarishaji wa miundombinu hiyo ambayo mingine imeanza kupasuka. Aidha, ameagiza shule hiyo kupelekewa miundombinu ya maji ili vyoo vilivyojengwa vianze kutumika badala ya kufungwa.Pamoja na kutembelea Shule ya Msingi Nguzo Mbili Mkuu wa Mkoa pia ameitembelea shule ya Sekondari na kukagua ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa vilivyojengwa kupitia mpango wa lipa kwa matokeo.
Mkoa wa Geita una upungufu wa vyumba vya madarasa 8600 hivyo serikali imeandaa mpango kabambe wa kutokomeza tatizo hili kwa kushirikiana na jamii na wadau wote wa Mkoa katika ujenzi wa vyumba vya madarasa.
NA: Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa