Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel ameendelea kupokea wageni mbalimbali wenye nia ya kuwekeza ndani ya Mkoa wa Geita katika kufanikisha azma ya Serikali ya Awamu ya Tano, yaani Tanzania ya Viwanda.
Miongoni mwa wawekezaji waliofika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita ni Mhe. Wasswa Lule kutoka Kampala Nchini Uganda na aliyewahi kuwa Mbunge aliyeambatana na wenzake watatu , lengo lake ikiwa ni kuwekeza kwenye kiwanda cha kusindika Maziwa ndani ya Mkoa huu.
Akiukaribisha ugeni huo, Mhe. Mhandisi Gabriel amemhakikishia mwekezaji huyo mazingira bora ya uwekezaji kwa kusema, “ hujakosea kuichagua Geita kama sehemu sahihi ya uwekezaji kwani mazingira mazuri kwa ajili yako na wawekezaji wengine wema yapo. Na hongera maana umewahi, kwani kwa sasa wawekezaji wanapiga hodi kila kukicha na milango bado ipo wazi”.
Kwa kutambua nafasi ya mwekezaji, Serikali imetoa eneo lenye ukubwa wa Ekari Nane kwa mwekezaji huyo ili kuharakisha uwekezaji ambao utakuwa na tija kwa kutoa ajira kwa wakazi wa Geita lakini pia kukuza uchumi wan nchi.
Akishukuru kwa niaba ya ugeni wao huo, Bw. Mahboob Mohamed alimshukuru Mkuu wa Mkoa na timu yake kwa ushirkiano na kuhakikisha wawekezaji hawakwami na wanapata mazingira rafiki ya uwekezaji.
Hivyo basi, bado wawekezaji mnaalikwa kuwekeza katika sekta mbalimbali kama viwanda vya maziwa, mchele, nyama, sukari, dhahabu n.k kwani Mkoa unatoa kipaumbele kwa wawekezaji wenye nia njema kwa ustawi na maendeleo ya Mkoa na Nchi kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa