Ikiwa ni mwendelezo wa vikao vya mikutano maalum ya mabaraza ya madiwani kujadili hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG), halmashauri ya wilaya ya Geita imepongezwa kufuatia kuwa na hati inayoridhisha kwa mwaka wa fedha 2020/21.
Pongezi hizo zimetolewa na mkuu wa mkoa wa Geita Mhe.Rosemary Senyamule Juni 23, 2022 wakati akiongoza kikao hicho ambapo msisitizo wake mkubwa umekuwa ni kuwachukulia hatua wale wote ambao husababisha hoja kwa uzembe, wote wanaokusanya mapato na kutokuyawasilisha na kisha kuhimiza viongozi kujipanga kupokea fedha nyingi za miradi ya maendeleo lakini pia kujipanga na Siku ya Samia mkoani Geita kwa kuhakikisha pia madiwani wanakuwa sehemu ya kutangaza mengi mazuri yanayofanywa na serikali.
“kwanza tumshukuru sana Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha nyingi za miradi. Pili niwapongeze kwa kupata hati safi pongezi ambazo ni za Halmashauri zote za mkoa huu bila kuacha kuwapongeza kwa kukusanya mapato na kuvuka lengo kwa kuwa na asilimia 105 hadi kufikia mwezi Mei,2022" amesema.
Ameongeza kuwa, " hoja za manunuzi ndizo zimeonekana kuwa nyingi, hivyo ni vyema kushughulikia eneo hili na vikao vya kamati ya ukaguzi viendelee kukaa kila robo ili wanaosababisha hoja wawajibishwe na pia Madiwani msaidie msukumo wa waliokopeshwa fedha ya 10% ya mapato ya ndani kurejesha ili wengine pia wakope"
Aidha RC Senyamule amesema, mkoa una andaa siku ya Samia ambayo itafanyika wiki ijayo lengo likiwa ni kuwaeleza Wananchi mafanikio na mambo mazuri yaliyofanywa na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan, kisha kwenda ngazi ya Wilaya, kisha kuwakumbusha wajumbe wa kikao hicho kujiandaa na Mbio za Mwenge wa Uhuru pamoja na zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.
Akimaliza wakati wa kuahirishwa kikao Mhe.Senyamule amekumbusha juu ya suala la chakula kwa watoto wa shule kama njia mojawapo ya kupunguza na kutokomeza utoro na kuwataka watumishi wote kuzingatia sheria, taratibu na kanuni katika utendaji wao.
Awali, mkaguzi mkuu wa nje (M) Geita CPA Richson Ringo baada ya kuwasilisha taarifa yake, aliwashukuru Geita DC kwa ushirikiano na kusisitiza juu ya uzingatiaji sheria mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa ukiukwaji wake ndiyo umepelekea hoja nyingi mfano sheria ya manunuzi.
CPA Ringo amewashauri madiwani wa halmashauri hiyo kufatilia vyanzo vya mapato kwa ukaribu na kupeleka ushauri kwa menejimenti ili kupata mapato stahiki lakini pia menejimenti kuepuka kutumia fedha za miradi ya Maendeleo kwenye shughuli nyingine.
Katika kikao hicho kaimu katibu tawala mkoa Bw.Herman Matemu amesema ni vyema Geita DC kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani ikiwemo kuhakikisha malipo yanayolipwa yote yawe yamehakikiwa na pia amesisitiza juu ya malipo yote kuzingatia sheria, taratibu na kanuni.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Geita Mhe.Wilson Shimo ametoa pongezi zake kwa Geita DC pamoja na kusisitiza kuweka mkazo mkubwa kushughulikia hoja hizo ili wakati ujao ziwe zimekwisha lakini pia kushukuru kwa ushirikiano wanaupata kutoka ofisi ya mkaguzi wa nje.
Naye Bi.Sania Mwangakala ambaye ni katibu tawala serikali za mitaa ameipongeza Geita DC kwa hati safi na ofisi ya mkaguzi kwa ushirikiano na kuwasihi kuanzisha vyanzi vya kudumu na si kutegemea madini tu ambayo hayana hakika ya kuwepo muda mrefu. Pia amewashauri kuwa na tamaduni ya kuandika maandiko ya miradi ili kupata fedha kujenga miradi mkakati
Hata hivyo mwenyekiti wa CCM wilaya ya Geita mhe.Barnabas Mapande ameanza kwa kuipongeza Geita DC kwa hati safi na kwamba hiyo ni kutokana na ushirikiano uliopo kati ya ofisi ya mkaguzi, ya mkurugenzi na madiwani.
Mwisho, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo mhe.Charles Kazungu amesema wataendelea kuifanya agenda ya hoja hizo kuwa ya kudumu kama mkakati wa kuzimaliza lakini pia amewasihi madiwani kuacha kuingilia zoezi la kuwafuatiliwa wadaiwa wa mikopo ya 10% akisema " achenill fedha za umma zirudi" lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi wengine kupata fedha hizo kisha kumaliza kwa kutoa pendekezo la kuwa na mradi wa kimkakati utakaopunguza umaskini kuliko kutoa fedha kidogo kwa watu wachache
Boazi Mazigo
Ag.HGCU
Juni 23, 2022
GEITA.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa