Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (Mb) amekabidhi Tuzo ya Ngao kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale baada ya kuibuka mshindi wa kwanza kwa kupata zaidi ya nyota tatu katika vituo vyake vyote vya kutolea huduma za afya Mkoani Geita. Ni katika ziara yake ya kikazi Mkoani Geita aliyoianza tarehe 26.07.2018.
Amesema “naipongeza Nyang’hwale kwa kupata asilimia tisini na tatu (93%) ya utoaji huduma bora za afya kwa maana ya kupata nyota kuanzia nyota tatu na kuendelea kwa kuwa pamoja na uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya afya ambayo serikali ya awamu ya tano imeufanya, sasa tunapima ubora wa huduma zinazotolewa”.
Amesema Geita ni mkoa wa tano katika ziara yake inayolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya afya ambapo lengo la serikali kwa sasa ni kuhakikisha vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinapata kuanzia nyota tatu na kuendelea kwenye upande wa utoaji huduma bora za afya.
Pamoja na hayo, Dkt. Ndugulile ameeleza masikitiko yake kuhusu mimba za utotoni ambapo amesema wale wote watakaohusika kuanzia mzazi, mwalimu na wahusika wengine juu ya kuharibu maisha ya mtoto, wakamatwe na wawajibishwe kwa mujibu wa sheria. Pia ameshauri kamati ya Ulinzi na Usalama isaidiee kufanikisha suala hilo na ikiwezekana kesi za watoto zisizidi miezi miwili na kuwahimiza wazazi kutowafanya watoto kama mitaji yao kwa kupokea mahari na kuwaozesha lakini wengine wakiwatumikisha bila kusahahau kuanzisha kamati za ulinzi wa mama na mtoto kama njia moja wapo ya uzimamizi.
Amesema pia ni muhimu kwa serikali ya mkoa kutoa muongozo wa vipaumbele kwa taasisi zisizo za kiserikali zinazotarajia kufanya miradi yao kwenye mikoa husika kwani mkoa ndio unayajua mahitaji yake na pia walete taarifa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amemshukuru Mhe. Naibu Waziri kwa ujio wake na kuhaidi kutekeleza maelekezo na kuongeza jitihada ili kufikia lengo la serikali kwa vituo vya kutolea huduma za afya mkoani kuwa na ubora wa kuanzia nyota tatu na kuendelea lakini pia amewapongeza Nyang’hwale kwa kujipatia tuzo hiyo na kuweka alama mkoani Geita hivyo wao ni chachu kwa mkoa na wengine waige waongezw bidii.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Joseph Odero ameeleza kuwa Hospitali ya Mkoa ina jumla ya watumishi 286 ambayo ni sawa na 42% na upungufu ni watumishi 395 ni sawa na 58% kulingana na ikama watumishi wanaohitajika katika Hospitali ya Mkoa ambao ni watumishi 681. Aliendelea kwa kutaja mafanikio yaliyopatikana yakiwepo kuimarika kwa hali ya Ubora wa utoaji wa huduma za afya vituoni kutokana na tathimni ya ubora wa huduma (health facilities star ranting) kutoka 42% mwaka 2015 ya vituo vyenye nyota hadi kufikia asilimia 98% mwaka 2017.
Matokeo ya Halmashauri za Mkoa wa Geita katika utoaji bora wa huduma za afya ni kama ifuatavyo;
1. Nyang’hwale – 93%
2. Mbogwe – 61%
3. Chato – 43%
4. Geita TC – 35%
5. Geita DC – 17%
6. Bukombe DC – 16%
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa