Programu ya IMASA Kuwainua Wananchi Kiuchumi Geita
Uanzishwaji wa program ya Imarisha Uchumi na mama Samia (IMASA) katika Mkoa wa Geita kutawezesha Zaidi ya wananchi elfu 64 kuinuka kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji mali wanazozifanya.
Kauli hiyo imebainishwa na Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala ya wanawake na makundi maalum Ndugu Sophia Mjema alipokuwa akizungumza na wanavikundi walioshiriki hafla fupi ya kutambulisha programu ya IMASA Mkoani Geita tarehe 20/9/2024 katika ukumbi wa GEDECO Geita mjini.
Ndg. Sophia Mjema ameeleza kuwa ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona kila mwananchi anaunganishwa katika mnyororo wa kukuza uchumi kupitia bidhaa wanazozalisha, hivyo amewaagiza wao kama wajumbe wanaozunguka Nchi nzima kwa lengo la kutembelea na kuzungumza na wanachama wa majukwaa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi sambamba na kukagua shughuli zinazofanywa na majukwaa hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali watanzania wakiwemo wananchi wa Mkoa wa Geita kupitia fursa za kiuchumi kama IMASA na kuahidi kushirikiana na viongozi wa majukwaa kubaini shughuli zote zinazofanywa na wanavikundi, changamoto zinazowakabili sambamba na kuibua fursa zilizopo katika jamii.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe.Louis Bura ametoa ushauri kutengenezwa kwa mfumo rasmi ambao utawawezesha wakulima, wafugaji na wajasiriamali wadogo kupata fursa ya kukopeshwa mikopo isiyo na riba ambayo itawainua na kufikia hatua ya kufanya shughuli zenye tija. Pia ameziomba taasisi za kifedha kurahisisha mchakato wa upatikanaji wa mikopo ili kuendana na msimu wa kila biashara, kilimo nk.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara , Mwenyekiti wa Chemba ya wafanyabiashara Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amemshukuru Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kila mwananchi anainuka kiuchumi kupitia fursa mbalimbali kama IMASA na kutoa mikopo yenye riba nafuu
Mhandisi Robert Gabriel ameongeza kuwa wao kama wafanyabiashara watajitoa kwa hali na mali katika kushirikiana na viongozi wa majukwaa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’i Issa amesema kuwa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara, wajasiriamali kwa sehemu kubwa ni kutorasimisha biashara zao na ukosefu wa mafunzo wa mifumo mbalimbali inayotumika katika uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
Bi. Beng’i Issa ameeleza kuwa program ya IMASA itahusika na uwezeshaji wa wanawake, vijana na makundi maalum katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na ile ya Tanzania visiwani ambapo program hiyo itaendeshwa kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Julai 2024 hadi Juni 2025 na itahusisha wanufaika Zaidi ya elfu sitini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa