Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe Uhuru Muigai Kenyatta amewasili nchini Tanzania julai 05, 2019 kupitia uwanja wa ndege wa chato, wilayani chato mkoani geita kwa lengo la kumtembelea Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
Katika salamu zake fupi kwa wananchi, Mhe. Kenyatta amesema kuwa, ni vigumu kwa yeyote kuitenganisha Kenya na Tanzania kutokana na ukweli usiopingika kuwa, nchi hizi mbila zina historia vilevile ni jirani na rafiki. Amesema pia mtu anaweza chagua rafiki ila si jirani, hivyo anashukuru Mungu kwa kuwa na jirani ambaye pia ni rafiki yaani nchi ya tanzania
Mhe. Kenyatta amesema “ninayo furaha kuwa rais wa kwanza kutoka nje ya Tanzania kutua katika uwanja huu wa ndege, lakini pia uwepo wa uwanja huu ni kwamba biashara itafunguka, viwanda vitajengwa, ajira zitapatikana. Niwaeleze tu kuwa, Kenya na Tanzania ni ndugu na hakuna atakayeweza kuigawa na kwa hii ndiyo jumuiya ya Afrika Mashariki tunayoitaka na si ya wenye firka ndogo, pia nashukuru kwa mapokezi makubwa kwakuwa nimehisi Tanzania yote imehamia chato”.
Rais Kenyatta amesema anampongeza Rais Magufuli kwa jinsi anavyowatengenezea watanzania miundombinu ya elimu, afya na maji huku akisisitiza kufanya kazi na kuacha kupiga siasa kila wakati akisema “tupunguze siasa, tujipange kwa maendeleo. Rais huyo ameeleza kuwa anaamini ipo siku timu ya Taifa Stars ya Tanzania na Harambee Stars ya Kenya zitacheza fainali pamoja kwenye kombe la Afcon.
Rais Kenyatta ameahidi kufanya ziara ya kikazi tena nchini Tanzania ambapo amesema atatembelea maeneo mbalimbali.
Awali akimkaribisha mgeni wake, Rais wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli amempongeza Rais Kenyatta kuwa Rais wa kwanza mgeni kutua katika uwanja wa ndege wa chato huku akisifu kwa jinsi alivyoshughulikia kauli ya wanaotaka kuzigawa nchi hizi.
‘tunatakiwa kujua kuwa, maneno huwa ni sumu kali haswa kwa watu wanaotaka umaarufu rahisi, yatupasa kujua kuwa Kenya na Tanzania zina mahusiano mazuri hata kabla ya ukoloni, hivyo nahimiza tuendelee kushirikiana. Tunataka wanajumuiya ya afrika mashariki kuungana kufanya biashara kwani idadi kubwa ya watu ni miongoni mwa kichocheo cha uchumi” amesema Rais Magufuli.
Hakuishia hapo, Rais Magufuli ametoa rai yake juu ya meli inayojengwa akisema hategemei meli hiyo kufanya safari zake Mwanza na Bukoba, bali hata Kenya ili tufanye biashara.
Naye mkuu wa mkoa wa geita mhandisi Robert Gabriel hakusita kueleza na kupambanua namna mkoa umejindaa kuwekeza kiuchumi ili kufuta takwimu inayousoma mkoa kama miongoni mwa mikoa iliyo na kiwango kikubwa cha umaskini ukizingatia utajiri uliyopo akimhakikishia uwepo wa kituo cha utalii, ukanda wa uwekezaji na masoko ya dhahabu vitaongeza pato la taifa huku akiomba kupewa watumishi wa idara ya madini ili kuongeza ukusanyaji wa mapato kwenye sekta hiyo
Mapokezi hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, chama na serikali wakiwemo wakuu wa mikoa jirani kama Mwanza, Shinyanga, Kagera na Kigoma ,mawaziri, naibu waziri, wabunge, madiwani, wakurugenzi wa taasisi mbalimbali, wananchi, bila kusahau wakuu wa wilaya.
Pia burudani mbalimbali zilizoandaliwa zilifana kiasi cha kuvutia umati wa wengi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa