Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema serikali itaendeleza miradi na shughuli zote zilizoasisiwa na Hayati Dkt Magufuli ikiwa ni sehemu ya kumuenzi kwani alitamani kuona Taifa linajitegemea na kukua kiuchumi.
Mhe. Rais Samia amesema hayo leo Machi 17, 2022 wakati wa Ibada ya misa Takatifu ya kumbukizi ya mwaka mmoja tangu kifo cha aliyekua Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli iliyofanyika kwenye uwanja wa Magufuli wilayani Chato.
Ameongeza kwa kubainisha kuwa ujenzi wa hospitali ya rufaa ya kanda, Kiwanja cha ndege cha Mkoa, Meli na Stendi ya mabasi iliyopo wilayani Chato ni baadhi ya miradi Mhe. Rais itakayoendelezwa na akatoa wito kwa watanzania kushikamana katika kuliletea Taifa maendeleo.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kushiriki kwenye zoezi la kitaifa la kutambua na kuweka anuani za makazi linaloendela nchini na baadae mwaka huu kushiriki sensa ya watu na makazi na walemavu wasifichwe bali wahesabiwe. "Tujitokeze wote, kila anayeitwa mtu ahesabiwe kwenye ziezi la sensa ya watu na makazi"
Dkt. Philip Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema Hayati magufuli aliwafundisha watanzania kufanya kazi kwa bidii ili kujitegemea na alijitoa nafsi yake kwa ajili ya Taifa hilo.
"Hayati Rais Magufuli alikua mwalimu wangu na naweza kusema kwamba alikua Mwalimu wa Taifa zima, alitufundisha kumtegemea Mungu na hata kwenye magumu kama magonjwa hakuchoka kutufundisha kumtegemea Mungu wakati wote."
Akitoa salamu za Serikali ya mapinduzi Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Mwinyi amesema kuwa kifo cha Hayati Magufuli kimewagusa watu kwa huzuni kutokana na ujasiri wake na ametoa wito kwa watanzania kumuenzi kwa kutenda mema aliyowahusia wakati wa uhai wake.
"Njia bora ya kumkumbuka marehemu ni kuzingatia misingi ya kuchapa kazi, mshikamano na upendo wa kizalendo na kupiga vita vitendo ya rushwa, ufisadi na uzembe mahala pa kazi." Rais Mwinyi.
Spika wa Bunge Mhe. Dkt Tulia Akson amesema kwenye kumbukizi hiyo watanzania wanayo furaha kuona Taifa linasonga mbele hata baada ya kupitia kwenye huzuni kubwa ya kuondokewa na Dkt Magufuli. "Mhe. Rais Samia Hassan umetupitisha salama, mwaka ule ulikua na magumu mengi." Amesema.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.Prof. Ibrahim Juma amebainisha kuwa hayati Dkt Magufuli alikua bega kwa bega kuisaidia mahakama hata kwa suala la kuhamia Dodoma kama Makao Makuu ya nchi na akasema mambo mema yote aliyofanya enzi za uhai wake yatakua historia na kudumu kwenye maisha ya Mahakama nchini.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Mhe. Philip Mangula ametoa pole kwa familia ya Hayati Dkt magufuli na amewapongeza wananchi wote walioungana na familia ya Hayati Magufuli kwenye ibada ya misa takatifu ya kumuombea mpendwa wao.
Waziri wa Utumishi na Utawala bora, Mhe. Jenister Mhagama amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza vema taifa na kuwafanya watanzania wasonge mbele hata baada ya kifo cha Hayati Rais Magufuli.
Vilevile, ametoa salamu za pole kwa familia ya hayati Dkt Magufuli na ampongeza mama Janeth Magufuli mjane wa uvumilivu kwa ujasiri wakati wote wa kuondokewa na mpendwa wao kama familia.
Akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Senyamule ameishukuru familia ya hayati Dkt. John Magufuli kwa kuamua kufanya kumbukizi muhimu iliyowakutanisha watanzania kumkumbuka jemedari mzalendo.
"Sasa hivi hatupokei tena kumbukumbu hii kwa huzuni bali tunaipokea kwa ujasiri na ushindi mkubwa kwani wanachato na Geita wanamkumbuka Dkt Magufuli huku wakifurahia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kurudisha imani ya wananchi kwa serikali yao." amesema.
Vilevile, Mhe. Senyamule amesema zaidi ya Bilioni mia moja imetolewa mkoani Geita kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na hayo yamefanya wananchi watembee kifua mbele kwa kuwa na matumanini makubwa hata baada ya kifo cha Dkt. Magufuli.
Akiongoza ibada ya misa takatifu, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu na Askofu wa jimbo kuu Katoriki la Geita Dkt Flavian Kasala ametoa wito kwa watanzania kumuenzi Hayati Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuwa na imani na dira ya maisha kama tunu ya kusonga mbele kwani bila matendo itakua ni imani mfu.
Aidha, amesema kusanyiko la kumbukizi si lisiende bure bali tumwombee toba kiongozi wetu ambaye aliliongoza Taifa kwa uaminifu mkubwa na pia tuwaombee marehemu wengine.
Mama Janeth Magufuli, Mjane wa hayati Dkt. John Magufuli amemshukuru Rais Samia, serikali na watanzania kwa kuungana na familia kwenye kumbukizi ya mwaka mmoja tangu msiba wa mpendwa wao na kwamba wote kwa ujumla waneonesha heshma kubwa kwa familia hiyo.
Paul Zahoro
Geita RS.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa