Na Boaz Mazigo, Geita RS
Katibu tawala mkoa wa Geita bw. Mohamed Gombati ameishukuru bodi ya pamba kupitia balozi wa pamba nchini Aggrey Mwanri kufuatia mafunzo aliyoyatoa kwa maafisa ugani na wakulima wa halmashauri ya wilaya ya mbogwe lengo ikiwa ni kuhamasisha uzalishaji bora wa zao la Pamba lenye kauli mbiu "pamba ni dhahabu nyeupe"
Shukrani hizo amezitoa Novemba 23, 2023 wakati akihitimisha mafunzo kwa makundi hayo na kusema ni vyema viongozi kuhamasisha uzalishaji wa zao hilo kwakuwa ni la biashara na soko lipo.
"nikushukuru sana balozi Mwanri na bodi ya pamba kwa ujumla kwa kufundisha wataalam na wakulima wetu mbinu bora za uzalishaji wa zao hili. Pamba ni zao la biashara, hivyo ni wajibu wetu kuongeza nguvu na uwezo wetu katika uzalishaji wake. Tujitahidi angalau ndani ya miaka miwili tulime kilo milioni 20 na kila mmoja wetu angalau awe na heka moja ili tuwe mabalozi wa mfano kwakuwa pamba inaongeza ajira na kuondoa umasikini", alisema bw.Gombati.
Aliongeza kuwa, Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan anawapenda sana wananchi na ndiyo maana mbolea hupatikana kwa bei ya ruzuku ya serikali, vinyunyizi na dawa hupatikana bure, hivyo ni vyema maafisa ugani kutumia fursa hiyo kuhamasisha wakulima na wananchi kwa ujumla kuzalisha kwa ubora na viwango.
Bw.Gombati alimaliza kwa kutoa wito kwa maafisa ugani kuwa, kwa namna kiongozi wa nchi alivyoweka mazingira wezeshi, watumishi wana wajibu wa kumlipa kwa kufanya kazi kwa bidii.
Kwa upande wake Balozi wa zao la Pamba nchini Aggrey Mwanri alimpongeza sana mhe.Rais Samia kwa utoaji wa dawa bure na mbolea ya ruzuku, na kwamba ameweka mazingira wezeshi ikiwa lengo ni kuzalisha Tani milioni 1 ifikapo mwaka 2025 na endapo lengo hilo litafikiwa, Tanzania itakua nchi ya kwanza barani Afrika.
Mafunzo hayo yalihitimishwa kwa kuambatana na kiapo walichoapa wakulima na maafisa ugani kuwa mafunzo waliyopewa watayatumia ipasavyo ili kuleta matokeo.
Hakika, Pamba ni Dhahabu Nyeupe.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa