Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, ameagiza kufanyika uchunguzi kufuatia nyufa/mipasuko iliyoonekana kwenye Zahanati ya Nyanguku iliyopo Kata ya Nyanguku Halmashauri ya Mji Geita.
Hayo yamejiri alipokuwa njiani kuelekea katika ziara yake ya kikazi kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo aliyoianza leo tarehe 05.11.2018 itakayofanyika mkoa mzima hivyo kupita katika Zahanati hiyo na kushangazwa na mipasuko iliyopo kwenye majengo hayo yanayokadiriwa kugharimu takribani Milioni Mia Mbili likiwa yamefunguliwa mapema mwezi januari mwaka 2018.
Kufuatia nyufa hizo, Mhandisi Gabriel ameagiza kushikiliwa kwa aliyekuwa Kaimu Mtendaji wa Kata ya Nyanguku Bw. Dionis Lubiyu ili asaidie kutoa maelezo ni kwa nini ujenzi haukuzingatia mahitaji yaliyopo kwenye makadirio ya gharama za ujenzi (BOQ), vilevile kuwatafuta wote waliosimamia mradi huo wakiwemo wataalamu ili kurudisha fedha ya serikali iliyopotea hadi kuwakosesha huduma wananchi.
Amesema, “yatupasa kuzingatia kanuni za ujenzi, tuwe wazalendo, ndipo tutaweza kuwatendea haki wananchi wetu kupitia miradi hii, TAKUKURU shughulikia suala hili, vilevile timu ya Mkurugenzi mara moja ianze uchunguzi na shughuli zisiendelee kwakuwa majengo haya ni hatari kutumiwa”
Kufuatia hali hiyo, tayari Mkoa umeandaa mfumo wa kusimamia na kuthibiti miradi yote inayotekelezwa ndani ya mkoa ambapo majaribio yatafanyika Halmashauri ya Mji na kwamba mfumo huo utakuwa na taarifa na picha za hatua mbalimbali kuanzia vifaa vya ujenzi, msingi, maboma n.k kuwa utakuwa ni mfumo utakaoweza kusaidia usimamiaji kuepuka changamoto kama ya Nyanguku.
Vilevile Mhandisi Gabriel ameagiza kutengwa kwa eneo jingine kwa ajii ya zahanati ya wakazi wa eneo hilo kwa kuwa kwa sasa wananchi wanapata huduma za afya katika kituo cha afya Nyankumbu Mjini Geita huku akiagiza uchunguzi wa majengo yote ya elimu na afya ili kujiridhisha na ubora kuepuka madhara ya baadae, kisha kuendelea na ziara yake.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa