Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) ofisini kwake tarehe 18.07.2018, lengo ikiwa ni kuamsha ari ya chama hicho lakini pia kuzungumza nao ili kujua changamoto zinazowakabiri kwa lengo la kukuza uchumi wa Geita.
Mhe. Mhandisi Gabriel aliwaeleza TCCIA kuwa chama hicho kinapaswa kutambua kuwa wao ndiyo wenye fursa za mkoa hivyo jicho lao litumike kuona fursa hizo na kuzitangaza pote kwa manufaa ya wanageita lakini pia kuhakikisha uchumi wa Geita ukamatwe na Geita.
Amesema, “TCCIA amkeni, simameni washeni moto wa maendeleo na sisi kama serikali tutawaunga mkono” .Aliendele kusema, “katafuteni maeneo ya uwekezaji kupitia Halmashauri ya Mji kwa kuwa hapa ndipo makao makuu ya mkoa, muwaalike wawekezaji kama hapa hawapo wa kutosha ili tuone matunda”. Mhe. Mhandisi Gabriel amewahimiza kuongeza wanachama kama ilivyokuwa hapo awali, kwa kufanya hivyo chama kitaimarika.
Amewashauri wafanyabiashara kuimarisha huduma zao kwani muda si mrefu Geita itaitika kimaendeleo hivyo ubora wa huduma ni muhimu. Mkuu wa Mkoa anapenda kuona Geita ni kimbilio la watu, hivyo watengeneze mazingira mazuri ili wageni wanapokuja Geita wakose kisingizio na kuzilieleza fursa zilizopo kwenye kilimo, mifugo, viwanda kwa ujumla ambazo bado hazijafanyiwa kazi ipasavyo.
Ameendelea kwa kuwapa changamoto wafanya biashara wa Geita kujenga kumbi kubwa za mikutano, nyumba za kulala wageni za kutosha, hoteli za kisasa za ghorofa hata kwa kuungana kwa kuwa Geita itapokea wageni wengi mwaka huu kwani jukwaa la fursa za biashara litakalofanyika kuanzia tarehe 15-16.08.2018 litaleta wageni wengi na pengine kupelekea uwekezaji mkubwa kufuatia bila kusahau maonesho makubwa ya Teknolojia ya Uchenjuaji na Uchatakaji wa Madini ya Dhahabu na Vito vya Thamani yatakayofanyika kuanzia tarehe 24-29.09.2018.
Alimaliza kwa kuwaasa kuepuka migogoro kwenye chama kwani kuna wengine hawapendi kuona juhudi zao zikifanikiwa kupitia mfano huu “wapo wachochezi sawa na Unaposhika pembe za Ng’ombe, wenzako wanashika mkia, lakini kimya kimya mbaya wenu anakamua maziwa, hivyo mjiepushe nao”.
Kwa upande wake katibu tawala Mkoa wa Geita, Bw. Selestine Gesimba alisema, uimara wa TCCIA ndiyo utakaoleta maendeleo ya kiuchumi kwa kuwa kikao hiki kimekuwa ni kwa ajili ya kufufua ari mpya ya utendaji kutokana na ukimya wa muda mrefu.
Naye mwenyekiti wa TTCIA Mkoani Geita kwa niaba ya viongozi wenzake Eng. Chacha Wambura alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa wito wa kikao hicho kwakuwa kimewajenga hivyo wamuahidi kwenda kufanya kazi na hamasa zaidi kwa wafanyabiashara mkoani Geita ili waweze kujiunga na chama hicho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa