Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel ameendelea kutoa onyo kwa wote wanaoendelea kutorosha carbon zenye madini ya dhahabu na kuzipeleka nje ya Mkoa wa Geita. Ni baada ya kupokea taarifa ya Mapendekezo ya Jinsi ya Kuratibu na Kuthibiti Shughuli za Uchimbaji, Uchenjuaji na Biashara ya Madini ya Dhahabu Mkoa wa Geita kutoka kwenye Kamati aliyoiunda tarehe 12.04.2018 yenye wajumbe kumi na tano (15) kutoka mbalimbali kama TAKUKURU, Jeshi la Polisi Ofisi za Madini Mkoa, RS Geita n.k iliyomaliza muda wake tahere 22.06.2018
Awali Mhe. Mhandisi Gabriel alianza kwa kuipongeza kamati kwa kazi nzuri waliyoifanya akisema ana imani nayo na kupokea mapendekezo waliyoyatoa lengo ikiwa ni kuokoa mapato ya Serikali yaliyopotea kwa muda mrefu.
Miongoni mwa mambo ambayo kamati iliyoyabaini ni pamoja na wafanya biashara kusafirisha carbon nje ya Mkoa wa Geita kwa kutoa sababu kwamba Elution nyingi za Geita (majiko ya kuchomea dhahabu) hazina Maabara ambazo zingewasaidia wamiliki wa ‘carbon’ kutambua kiwango cha dhahabu (ppm au g/t) kilichomo ndani ya carbon, hivyo kuwa na uhakika juu ya kiwango cha dhahabu kitakachopatikana baada ya kufanyika uyeyushaji (smelting), jambo lililopelekea Mkuu wa Mkoa wa Geita kutolea ufafanuzi suala hilo akisema, “napenda kuwatoa hofu wafanya biashara wote wa dhahabu kuwa , kwa sasa Mkoa wa Geita una Elution zenye uwezo kwa kushugulikia jumla ya tani kumi (10) za Carbon kwa siku kwa Teknolojia ya kisasa ya High Pressure yenye uwezo wa kuchoma carbon kwa masaa ishirini na nne (24) na ya gharama nafuu tofauti na Teknolojia ya zamani ya Low Pressure inayotumia masaa 48-55 yenye gharama kubwa za uendeshaji na nyingine zinajengwa, lakini pia kamera za Usalama (CCTV) zimefungwa hivyo kumhakikishia usalama wa uzalishaji katika Elution hizo”. Pia alitoa onyo kwa wote wanaotorosha carbon kupitia magari na kuagiza kuwa, endapo watatokea watu wataokamatwa wakitorosha carbon, itumike Sheria ya Madini ya Tanzania, Sheria namba 14 ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 ambapo atakayekamatwa, atalipa faini isiyopungua Milioni Tano na Isiyozidi Milioni Kumi kwa mtu binafsi na Milioni Hamsini kwa kampuni pamoja na utaifishaji wa mali zao.
Mwisho, Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw. Mohamed A. Majaliwa na Katibu wake Bi. Asha Rajabu walimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwateua na kuiamini kamati yao hadi kupata taarifa itakayoweza kuusaidia Mkoa katika kupanga mikakati ya kuokoa mapato ya Serikali yaliyopotea muda mrefu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa