Ni tarehe ya pili ya mwezi wa kwanza mwaka 2019, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel anapata mwaliko wa kushiriki kazi ya jamii kutoka kwa Umoja wa Vijana CCM Wilaya ya Geita na Kuchimba msingi wa nyumba ya watumishi 2 kwa 1 katika Zahanati ya Ntono, Kata ya Bukoli, Halmashauri ya Wilaya Geita katika kuwaunga mkono vijana ndani umoja huo waliopo kwenye kambi iliyoandaliwa na viongozi wa UVCCM (W) Geita ikiwajenga vijana katika utamaduni wa kupenda kazi, kupinga rushwa pamoja na kuwa wazalendo.
Akiongea na washiriki wa kambi hilo pamoja na wananchi waliojitokeza kushiriki shughuli za uchimbaji msingi wa nyumba hiyo, Mhe. Mhandisi Gabriel amewapongeza juu ya uamuzi walioufanya huku akisema jambo hilo lafaa kuigwa na mkoa mzima huku akiwasihi kutangaza mazuri mengi yanayofanywa na viongozi wao, wayajivunie na wayaishi na kuwatakia heri ya mwaka mpya na kwamba mwaka huu ni wa kazi.
Amesema, “nawapongeza sana UVCCM Wilaya ya Geita kwa kuandaa kambi hili lenye kuleta matokeo, nawapongeza vijana washiriki wa kambi na wananchi kwa ujumla kwakuwa hapa mnawekeza kwa baadaye kwakuwa kesho zahanati hii ikifunguliwa, watakaotibiwa ni familia zenu wenyewe, hivyo yawapasa kujivunia hili na kutangaza habari hizi njema kuwahamasisha na wengine”.
Hakuishia hapo, bali pia amewasisitiza kuwa wazalendo kama ambavyo wamekuwa wakifundishwa kambini na kwamba mageuzi ya nchi kimaendeleo hufanywa na wananchi wenyewe ukizingatia kwamba, Mungu kaibariki Tanzania kwa kuipa kiongozi miongoni mwa viongozi bora na wachache duniani Mhe. Rais Dkt. Magufuli, hivyo ni vyema kufanya kazi ili kuleta maendeleo, kisha akaelekea Kijiji cha Ihega, Kata ya Bukoli na kushiriki kujenga msingi wa vyumba 3 vya madarasa, msingi uliochimbwa na vijana hao wa Umoja wa CCM Wilaya.
Baada ya Kutoka Ihega, Mkuu wa Mkoa aliekea kijiji cha Bugogo, Kata hiyo hiyo ya Bukoli na kuangalia ujenzi wa vyumba 3 vya madarasa vilivyojengwa hadi hatua ya madirisha na vijana wa umoja huo na baadaye kumaliza kwa kupanda mti aina ya Mkwaju katika Shule ya Sekondari ya Bukoli iliyopo kijiji cha Ikina kama ishara ya utunzaji mazingira na kumbukumbu ya wanakambi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Geita, Ndg.Manjale Magambo amemweleza Mkuu wa Mkoa kuwa, wao kama vijana wanaonyesha njia, wanaacha alama hivyo kuwashukuru wananchi waliojitokeza kuunga mkono juhudi walizozianzisha kama viongozi wa CCM ngazi ya wilaya kwakua wao ni watendaji na si wapiga maneno.
Diwani wa Kata ya Bukoli, Mhe. Rajab Seif akatumia fursa hiyo kumpongeza Mkuu wa Mkoa kwa ushiriki wake katika shughuli mbalimbali za maendeleo akisema “ mhe.Mkuu wa Mkoa, nilishasema na nitaendelea kusema kuwa, HUKULETWA GEITA KWA BAHATI MBAYA” huku akimpongeza kwa usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya jamii CSR iliyosaidia uezekaji wa miundombinu inayoendelea kujengwa.
Awali akitoa taarifa fupi, Mkuu wa Kambi na Katibu wa UVCCM (W) Geita Ndg.Ally Rajab, amemweleza Mkuu wa Mkoa kuwa, kambi hilo lilianza tarehe 27.12.2018 likiwa na jumla ya washiriki 112, lakini kutokana na kwamba linazingatia weledi na nidhamu, hadi sasa wamebaki vijana 101 tu na kusema tayari wameshiriki kuchimba misingi 6 na kujenga madarasa matatu hadi hatua ya madirisha na kuchimba shimo la choo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa