Ikiwa yamesalia masaa kadhaa kuelekea mtanange mkali unaotarajiwa kuchezwa katika uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza Novemba 21, 2020 kuanzia saa kumi jioni baina ya timu ya Geita Gold FC kutoka Geita inayomilikiwa na halmashauri ya mji Geita na timu ya Pamba FC ya Mwanza, mkuu wa mkoa wa Geita mhandisi Robert Gabriel leo Novemba 20, 2020 amefika ilipo kambi ya wachezaji wa timu hiyo ya Geita zilipo nyumba za NHC eneo la Magogo kwa lengo la kuwatia moyo na hamasa ili waweze kuwa washindi wa mchezo huo.
Akizingumza na wachezaji pamoja na viongozi wa timu hiyo, mhandisi Gabriel ameeleza kuwa, kupitia sura ya 242 hadi 243, ukurasa na. 291 hadi 294 wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020, tayari serikali ilielekezwa kuendeleza na kusimamia michezo katika ngazi mbalimbali nchini, hivyo kama kiongozi mkuu wa serikali mkoani geita, atahakikisha anatekeleza wajibu huo kama maelekezo yalivyotolewa.
“niwapongeze kwakuwa mmeanza vizuri na kiu yangu ni kuona maisha yenu yanaenda mbali zaidi. Ifike mahali ukiwa uwanjani usipoteze mpira kwakuwa unajua una wajibu mkiyajenga maisha yenu kupitia mpira na kama kiongozi tunaanza na utafutaji wa kiwanja kwaajili ya kocha kisha wachezaji mtafuata, hii yote ni katika kuhakikisha mpira unakuwa ni sehemu ya maisha yenu. Hivyo jueni mna deni kuutangaza mkoa nasi tuna deni kuwainua”, mhandisi Gabriel alieleza.
Pia, mkuu wa mkoa huyo alilisisitiza juu ya kuwa na tabia ya kuwekeza ikiwa tunataka matokeo mazuri huku akieleza kwa ufupi wasifu wa kocha wa sasa wa timu ya Geita Gold ndg. Fredy Minziro, kisha kumpigia simu mkuu wa wilaya ya geita ili aambatane na timu hiyo siku ya jumamosi ya Novemba 21, 2020 kwaniaba ya serikali ya mkoa katika mtanange huo.
Katika hatua nyingine, kocha wa timu hiyo ndg.Fredy Minziro alimshukuru mhandisi Gabriel kwa kuwatembelea na kuwatia moyo huku akiahidi ushindi wa kishindo akisema anaamini ushirikiano wanaoupata kutoka serikalini na kwa wadau mbalimbali utaisababisha timu hiyo kusonga mbele.
Akishukuru kwaniaba ya timu, nahodha Joseph Mwarabu alishukuru ujio wa RC Geita na kumsihi asiichoke timu hiyo na kwamba wanaamini watatimiza malengo yao ikiwemo ya kupanda daraja.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa timu ya Geita Gold Fc ya Geita kuchuana na timu ya Pamba FC ya Mwanza ili kuingia ligi kuu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa