Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, amekabidhi jumla ya Tv Screen tatu (3) na ving’amuzi vitatu (3) kwa washindi ambao ni wateja wa Benki ya CRDB tawi la Geita katika kampeni inayoendeshwa na Benki hiyo katika msimu huu wa Kombe la Dunia iitwayo “Shiriki Kombe la Dunia FIFA 2018 na Tembocard Visa.
Baada ya kukabidhi zawadi kwa washindi, Mhe. Mhandisi Gabriel alitoa pongezi kwa uongozi wa Benki hiyo kwa hamasa ambayo wamekuwa wakiitoa kwa wateja lakini pia kwa huduma muhimu kama hiyo ya malipo ya mtandao. Aliwashukuru kwa kuwahakikishia wateja usalama wa fedha zao kwani kwa kufanya hivyo wanalinda uhai wa wageni na wananchi wa Geita na kwa kuwa hawatakuwa wakitembea na fedha nyingi mifukoni.
Alisema “nawapongeza washindi wote, watumia huduma ya Malipo ya Mtandao lakini Meneja wa Benki hii na Wafanya kazi wenzake nawapongeza kwa kuwa mimi kama Mkuu wa Mkoa sijawahi kupokea malalamiko yoyote kutoka kwa wateja wenu juu ya huduma zenu ofisini kwangu, hivyo basi tabasamu wanaloingia nalo wateja kwenye Benki yenu hakikisheni linajizalisha mara mbili yake” kisha kukata keki pamoja na washindi.
Mhe. Mhandisi Gabriel, aliendelea kwa kutoa wito kwa taasisi mbalimbali zikiwemo za Afya pamoja na wananchi wa Geita kwa ujumla kujiunga na aina hiyo ya huduma kwani ni njia rahisi na salama, jambo linalothibitika kupitia taasisi chache zilizotajwa na Benki ya CRDB Geita kama watumiaji wa huduma hiyo.
Akitoa utangulizi wakati wa ufunguzi wa hafla hiyo fupi, Meneja wa Benki ya CRDB Tawi lilipo Mjini Geita Bw. Amini Mwakang’ata alisema, kampeni hiyo ilianza mwezi Aprili, 2018 na inatarajia kuhitimishwa Mwezi Julai, 2018 lengo ikiwa ni kuwahamasisha wateja wake kutumia huduma ya Malipo ya Kimtandao (Online Payments) kupitia Tembocard Visa inayomwezesha mteja kununua bidhaa hata kama hana fedha mfukoni, njia ambayo ni salama kwa mnunuaji na muuzaji. Aliendelea kwa kutaja taasisi ambazo tayari zimejiunga na huduma hiyo kuwa ni pamoja na RK Supermaket, Lenny Hotel pamoja na kituo cha mafuta kiitwacho Mwatulole Filling Station na kuwahimiza wale wote wanaosita kutumia huduma hizo basi wajiunge.
Bw. Mwakang’ata aliwataja washindi wa kampeni hiyo kuwa ni wananchi watatu wakazi wa Geita ambao ni ambao ni Bw. David Hugg, Meneja kampuni ya GPH ambaye pamoja na zawadi zilizotolewa ameshinda kwenda Nchini Urusi ambapo atashuhudia Nusu Fainali ya Kombe la Dunia, Mhandisi Jonas Maluku kutoka TANROADS Geita pamoja na Bw. Gerald Midenyo. Watumishi na washindi walimalizia kusherekea ushindi huo kwa burudani na kula keki iliyokuwa imeandaliwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa