Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amekutana na kufanya kikao na uongozi wa shule ya Sekondari ya binafsi (High School) Golden Ridge iliyoko Mjini Geita ili kujua ni kwanini wamekuwa miongoni mwa shule kumi za mwisho Kitaifa na kutia doa kwenye Mkoa ilihali Mkoa kwa sasa una jitihada za kuinua kiwango cha elimu na maisha ya wananchi kwa kuboresha miundombinu ya Elimu na Afya. Ni kufuatia taarifa ya matokeo ya kidato cha sita mwaka 2018 iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
Mhe. Mhandisi Gabriel amempa angalizo mkuu wa shule hiyo kwa kumshauri aepuke kupokea wanafunzi wa madarasa ya mtihani kama kidato cha nne na sita bila kuwapima na kujua uwezo wao, jambo ambalo lisipozingatiwa vizuri huleta athari kwenye matokeo ya mitihani hasa ya mwisho ya Kitaifa.
Amesema “mwalimu, nenda ukafanye mapinduzi kwenye shule yenu, zinatieni vigezo. Wafuatilieni wanafunzi wanaohamia shuleni kwenu, na wale wa madarasa ya mitihihani mjiridhishe na walikotoka lakini pia kwakuwa shule yenu ni ya mchanganyiko, mjitahidi kufuatilia maadili ya wanafunzi ili kusitokee athari zozote za kimaadili na kinidhamu”. Pia Mkuu wa Mkoa aliwaagiza wataalam wa idara ya Elimu Halmashauri ya Mji Geita kushirikiana na wataalamu wa elimu Ofisi ya Mkoa kupitia wadhibiti ubora wafanye ukaguzi kujiridhisha na ubora wa elimu inayotolewa na waalimu wa shule hiyo.
Akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Shule hiyo Mwl. William Kachinde alieleza kuwa, amefanya jitihada kubwa ilhali ni mgeni shuleni hapo na miongoni mwa sababu kubwa iliyosababisha anguko hilo kitaaluma kwenye matokeo ya kidato cha sita, ni kupokea wanafunzi wahamiaji kumi na mbili (12) wanaofanya jumla ya wanafunzi kumi na nne (14) kupata ziro kwenye matokeo hayo wavulana wakiwa 10 na wasichana 2. Ili kuweka kumbukumbu sahihi, Mwl. Kachinde alieleza kuwa kwa mujibu wa matokeo hayo, shule hiyo imekuwa ya mia tatu thelathini na nne (534) kati ya shule mia tano arobaini na tatu (543) Kitaifa na kuingia katika orodha shule kumi za mwisho. Kisha alihaidi kufuata ushauri uliotolewa ili hali hiyo isijirudie kwa kuwa wao kama shule pia hawakupenda kuteleza kwenye matokeo hayo.
Naye Kaimu Afisa Elimu wa Halmashauri ya Mji Geita Mwl. Ramadhan Khalfan amemweleza Mkuu wa Mkoa kuwa, kwa upande wake ameona sababu nyingine ni kitendo cha mmiliki wa shule kuwa na tabia kubadili wakuu wa shule hiyo mara kwa mara na ndani ya kipindi kifupi, jambo ambalo kiutawala lina athari na kusema wamekuwa wakikaa na uongozi wa shule hiyo kwa mashauriano na atatekeleza yote waliyoelekezwa ili kuondoa tatizo hilo.
Matokeo ya Shule ya Sekondari Golden Ridge ni kama ifuatavyo; (Div I=3, Div II=31, Div III=79, Div IV=21 na F au 0 =14), katika Jumla ya wanafunzi 154 waliofanya mtihani. Waliofaulu ni wanafunzi 134, wastani wa GPA ya 4.0428, na imekuwa shule ya kumi (10) kati ya shule (10) ndani ya Mkoa wa Geita.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa