RC GEITA - AUAGIZA UONGOZI WA HALMASHAURI YA MJI GEITA KUPELEKA WAKAGUZI WA HESABU ZA SERIKALI KATA YA MGUSU WILAYANI GEITA
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Modest Apolinary kupeleka Wakaguzi wa ndani wa Hesabu za Serikali Kata ya Mgusu ili wakakague na kujiridhisha na mapato na matumizi ya fedha mbalimbali katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Mgusu na Mtaa wa Machinjioni Wilayani Geita.
Mheshimiwa Robert amesema hayo wakati wa ziara yake Halmashauri ya Mji Geita yenye lengo la kuzindua kampeni ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na Zahanati ambapo baada ya uzinduzi kufanyika wananchi wa mtaa wa machinjioni walimueleza kero ya kutopata taarifa ya mapato na matumizi ya michango wanayochangia kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa muda mrefu katika mtaa wa Machinjioni na kata ya Mgusu.
Akijibu kero hiyo Mkuu wa Mkoa amesema "Kama kuna kiongozi wa mtaa au Kata amekula fedha za wananchi hafai kuwa kiongozi serikali itamchukulia hatua kali za kisheria na atarejesha fedha hizo!, Mkurugenzi leta timu ya ukaguzi wa hesabu za Serikali ili ikague na kujiridhisha kama kuna fedha yoyote iliyochukuliwa pasipo maelezo yanayojitosheleza hatua zichukuliwe haraka kwa wote watakaobainika kuhusika". Mheshimiwa Robert ameongeza kuwa ukaguzi huo ufanyike kuanzia mwaka 2014 hadi 2017 kisha apate taarifa hiyo ofisini. Akiwa katika Halmashauri hiyo Mkuu wa Mkoa amepongeza jitihada zinazofanywa na wananchi za kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo licha ya kuwepo changamoto nyingi katika maeneo yao.
Mkuu wa Mkoa amehitimisha ziara yake ya Mkoa mzima katika Halmashauri ya Mji Geita kwa kutembelea na kushirikiana na wananchi kujenga nyumba pacha ya walimu (Two in one) Shule ya Msingi Shinamwendwa, ujenzi wa kituo cha Zahanati Mtaa wa Nyakato , ujenzi wa vyumba vya madarasa viwili, ujenzi wa jengo la utawala shule ya Sekondari Mgusu pamoja na kukagua eneo la kujenga Zahanati katika Kata hiyo. Katika ziara hiyo ya Mkoa mzima Mheshimiwa Gabriel amefanikiwa kutembelea Wilaya zote tano (5) na Halmashauri sita(6) na kufanikiwa kujenga, kutembelea na kuanzisha jumla ya miradi 19 katika Sekta za Afya, Maji na Ujenzi huku akikusanya zaidi ya mifuko 800 ya Saruji, tofali za Block 500, Mbao 50. Haya yote ni matokeo ya kazi aliyoianza ya kushirikiana na wananchi kutekeleza miradi ya maendeleo katika kila kijiji ndani ya Mkoa huu lengo kuu likiwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora karibu na maeneo yao pia kupunguza uhaba wa vyumba vya madarasa na Zahanati Mkoani humu.
Wananchi wote katika maeneo aliyopita kufanya kazi wameonyesha kuridhishwa na utendaji kazi wa Serikali na kuamua kuunga mkono juhudi hizi kwa kushiriki katika utekelezaji wa miradi kama vile kuchota maji, kubeba mawe, mchanga, kokoto, kuchimba misingi na vijana kujitolea kujenga miradi hii.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa