Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel aagiza kukamatwa kwa Mtendaji wa Kijiji cha Nyahwiga Ndugu David Kabalu aliyetoroka na fedha za Michango ya Madawati Tshs. 250000/= na kutokomea kusikojulikana.
Mhe. mkuu wa Mkoa ametoa maagizo hayo leo tarehe 03 Februari, 2021 kwenye shule ya Sekondari ya Masumbwe Wilayani Mbogwe wakati wa Mkutano wa Majumuisho ya ziara yake Wilayani humo ambayo ametumia siku nne kutembelea Miradi ya Afya na Elimu hususani kutatua kero ya Miundombinu ya Madarasa, Zahanati,Matundu ya Vyoo, Nyumba za Walimu, maabara, mabweni, mabwalo ya chakula, Viti na Meza kwa Wanafunzi.
Aidha, ameagiza kuchukuliwa ahatua za kinidhamu Mtendaji wa Kata ya Nhomolwa kwa kushindwa kusimamia majukumu yake ya kazi kikamilifu kama vile usimamizi wa Watendaji wa Vijiji na kusababisha kutokamilika kwa Miradi kwenye kata hiyo kama ilivyothibitishwa kwenye Ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kabanga kwenye kata hiyo uliokwama kwa miaka kumi pamoja na kufikia hatua ya Ukamilishwaji juhudi zilizofanywa na wananchi tena hali hiyo imeendelea hata baada ya mwezi wa Septemba 2020 kuopatiwa vifaa vya kukamilisha ujenzi wa Zahanati hiyo lakini vifaa hivyo kama saruji na Dari vinaharibika viiwa bado vimehifadhiwa ndani.
Kufuatia hali hiyo Mhe. Mkuu wa Mkoa amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kumbadilishia kazi Mtendaji wa Kijiji cha Kabanga kwani anaonekana ameshindwa kumudu majukumu hayo kutokana na hali ya uzee aliyo nayo. Vilevile, ameitaka Halmashauri ya wilaya ya Mbogwe kuhakikisha wanavitumia vifaa hivyo ndani ya juma moja kwani wasipofanya hivyo atavigawa kwenye kata zingine zikatekeleze Miradi mingine.
“kuna changamoto ya uwajibikaji kwa watumishi hapa, kwenye Kata moja nimelalamikiwa Mtendaji wa kata anaishi Shinyanga Wilayani Kahama na haonekani kwenye kata yake na ndani ya kata hiyohiyo kijiji kimoja Mtendaji amekimbia na fedha za Madawati sasa naagiza akamatwe.” Amesema Mkuu wa Mkoa.
Wakati huohuo, Mhe. Mkuu wa Mkoa ameziagiza Taasisi ya Kupambana na Kuthibiti Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani Wilayani Mbogwe kufanya ukaguzi kwenye Matumizi ya Fedha Milioni 56 zilizotumika kabla ya kuundwa kwa kamati ya Ujenzi wala ya Mapokezi kati ya Milioni 400 zilizoletwa Na TAMISEMI kwa ajili ya Ujenzi wa madarasa kwenye shule ya Msingi Kasandalala.
Mhe. Gabriel amewataka Halmashauri kuwa wawazi kwenye shughuli za Ujenzi kwenye madarasa ya Shule zote kwa kuichambua BOQ kwa watu wote wanaohusika na ujenzi na amewataka kuhakikisha ndani ya juma moja walipe madeni ya mfundi wanayodai kwenye kazi za siku za nyuma.
Katika hali isiyo ya kawaida, Mhe. Mkuu wa Mkoa amebaini kwamba Fedha za mapato ya ndani kwenye Halmashauri ya Mbogwe hazijapelekwa kabisa kwenye Miradi ya Elimu Wilyani humo tangia mwaka wa fedha ulipoanza pamoja na kukusanya zaidi ya Milioni 600 ndani ya miezi sita ya mwaka 2020/2021. Kwenye hilo Mhe. Gabriel ameagiza Halmashauri hiyo kuheshimu taratibu za mapato na matumizi ya Fedha za Halmashauri ili waweze kuwaletea wananchi maendeleo. “Halmashsuri hii mnanishangaza ,kama Elimu sio kipaumbele chenu, niambieni ni nini kipaumbele chenu.” Alihoji Mhe. Mkuu wa Mkoa.
Pamoja na ujenzi wa Madarasa, kufuatia Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kasandalala kuwa zaidi ya elfu nne Mhe. Mkuu wa Mkoa amewataka Halmashrui ya Wilya ya Mbogwe kujenga shule mpya jirani na shule hiyo ili kupunguza Msomngamano shuleni hapo.
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Geita amehitimisha Ziara ya Kutatua kero ya Msongamano kwenye shule za Sekondari Wilayani Mbogwe ambayo ametembelea shule zote 16 za Sekondari na Zahanati pamoja na vituo vya kutolea huduma za Afya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa