Na Boaz Mazigo, Geita RS
Mkuu wa mkoa Geita Mhe.Martine Shigela ametoa salam za pole za Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya wilaya ya Chato walioathirika kufuatia mvua kubwa nayoendelea kunyesha kama ambavyo ilitahadharishwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini TMA juu ya uwepo wa mvua za Elnino.
Ametoa salamu hizo za pole Novemba 28, 2023 alipofanya ziara wilayani humo kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Kitongoji cha Zakia, Kitongoji cha Ibanda, Kata ya Muganza na kujionea uharibifu wa mali na miundombinu kisha kuwashukuru viongozi na wananchi kwa hatua za awali za kuwasaidia waathirika hao pamoja na kuwahimiza kuendelea kuchukua tahadhari.
"kwanza nifikishe salamu za upendo za pole kutoka kwa kiongozi wetu na Rais wetu Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kufuatia maafa yaliyotokea. Kwaniaba ya serikali nitatoa kwa kuanzia kilo 300 za Unga wa Mahindi ya chakula ili angalau wakati tunasubiri takwimu za waathirika ziwasaidie. Vilevile niwashukuru wana Chato kwa moyo wa upendo wa kuwasaidia wenzenu ambao wamekosa malazi mkawapa hifadhi na kwa wale waliojeruhiwa, serikali itagharamia matibabu yao yanayostahili", alisema RC Shigela.
Aliongeza kuwa, ni vyema wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa wale wote mnaoishi kwenye mabonde au jirani na mabwawa na kama Serikali inao mpango wa kufungua barabara za kwenye vitongoji ili muda utakapofika wananchi wawe tayari kutoa ushirikiano bila kudai fidia.
RC Shigela alihitimisha kwa kumuelekeza mkandarasi ambaye anarekebisha barabara kuhakikisha afanya kazi hiyo ndani ya muda ili kuokoa miundombinu hiyo.
Kwa upande wao waathirika wa mvua hiyo walisema wanaishukuru serikali na Mhe.Rais Samia kupitia mkuu wa mkoa kwa kuwatembelea na kuwajulia hali na kuwapa msaada.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Mkoa na Wilaya
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa