Na Boazi Mazigo-Geita RS
Serikali mkoani hapa imeeleza kuwa, inatambua na kuthamini mchango wa waandishi wa habari na kueleza kuwa msimamo wake ni watumishi kuendelea kutoa ushirikiano na kutoa majibu kwa waandishi wa habari kwa wakati ili kuondoa sintofahamu zinazoweza kutokea kutokana na kutokutoa majibu kwa wakati.
Hayo yameelezwa Oktoba 17, 2023 na mkuu wa mkoa wa Geita Mhe.Martine Shigela wakati akiahirisha warsha ya siku moja iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Geita iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa kisha kuipongeza TCRA kufuatia maandalizi na kufanyika kwa warsha hiyo.
“kwanza niwapongeze TCRA kwa hili mlilolifanya, lakini kwenu waandishi niwaeleze kuwa, serikali inamthamini mwandishi wa habari kwakuwa ninyi ni miongoni mwa nguzo muhimu kwenye utawala wa sheria na kupitia dhamira ya Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan ya haki, uwazi na demokrasia ndiyo maana mpo huru kutekeleza majukumu yenu” alisema RC Shigela.
Aliongeza kuwa, waandishi wa habari ni watu muhimu kwakuwa husaidia kuonesha fursa za maendeleo kwa watu ambao hawajazifahamu fursa hizo na hivyo kutoa wito kwa chama cha waandishi wa habari Geita GPC wahakikishe wanatoa ushirikiano na kwamba kama serikali ya mkoa itawaunga mkono ili kufanikisha malengo yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Geita (GPC) Renatus Masuguliko aliahidi na kutoa wito kwa wananchama kuwa, anaendelea kuwakaribisha waandishi kuwa wananchama na kwamba waandishi ni vyema kutekeleza wajibu, sheria, taratibu, sera na miongozo katika kutekeleza majukumu yao ili wasijeingia kwenye mikono ya sheria kutokana na kuenenda tofauti na sheria, kisha kuahidi kuyafanyia kazi mafunzo yote yaliyotolewa ikiwemo uzingatiaji suala la taaluma kwa waandishi wa habari.
Naye Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo alisema, kukutana na waandishi hao wa habari ni moja ya utekelezaji wa jukumu la TCRA la usimamizi na ufuatiliaji wa maudhui ya utangazaji na uandishi wa habari wakifuatilia waandishi wa habari na vyombo vya habari ikiwa wanakidhi matakwa ya sheria, kanuni, misingi na maadili ya uandishi wa habari na kuwasihi kuzingatia yote waliyokumbushwa.
Warsha hiyo ilihudhuriwa na waandishi wa habari kutoka halmashauri zote za mkoa wa Geita pamoja na maafisa habari.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa