Na Boazi Mazigo -Geita
Hadi hivi leo Agosti 11, 2022 zimesalia siku 12 tu kufikia Sensa ya Watu na Makazi ambapo Mkuu wa Mkoa Geita Mhe.Martin Shigela amekabidhi jumla ya Pikipiki 8 aina ya TVS kwa Vyombo vya Kijamii vya Watumiaji Maji CBWSOs zilizotolewa na Serikali ya Tanzania (Wizara ya Maji) kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA Mkoa wa Geita.
Akizungumza kabla ya kukata utepe na kukabidhi pikipiki hizo, Mhe.Shigela ameanza kwa kuishukuru na kuipongeza Serikali chini ya Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyoimarisha utendaji wa kazi wa wataalam kupitia uwezeshaji wa vitendea kazi ikiwemo magari na pikipiki kwenye sekta ya maji bila kusahau utoaji wa fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali ya maji ikiwemo akitoa mfano kwa Mkoa wa Geita kupokea Bilioni 18 kwa mwaka wa fedha 2021/22 na zaidi ya Bilioni 11 kutoka fedha za ndani (GoT na NWF) na PforR kwa mwaka wa fedha 2022/23 bila kusahau mradi wa Takribani Bilioni 100 kwa chanzo cha Ziwa Viktoria kupitia Benki ya Exim India utakaonufaisha mji wa Geita.
Mhe.Shigela ametahadharisha watu wasio waadilifu wenye nia ya kutumia kinyume na kusudio vitendea kazi hivyo akisema, “ni vyema kuzitunza pikipiki hizi, zifanye kazi kusudiwa na zisifanye biashara ili zilete matunda kusudiwa na serikali ya awamu ya sita”
Pia Mhe.Shigela ameeleza kuwa, wizara tayari imetoa miongozo itakayozingatiwa na wananchi na watumiaji maji watakaochota kwenye maeneo ya jumuiya akisema, “maji ambayo hupatikana kupitia msukumo wa mashine zinazotumia mafuta ya Dizeli, yatauzwa Sh.50 kwa ndoo, yale yatokanayo msukumo wa mashine zinazotumia umeme wa TANESCO au REA yauzwe Sh.40 kwa ndoo na yale yanayotokana na msukumo wa Jua, ndoo isizidi Sh.30 na yale kwa njia ya Pampu za mkono pamoja na mseleleko (Gravity), ndoo itauzwa Sh.25, ruksa kushusha na hata wale wenye bei za chini msipandishe kiholela bila kufuata taratibu”
Mhe.Shigela amemaliza kwa kuwahakikishia ushirikiano kutoka ofisi anayoiongoza na kuwataka watumishi wa sekta ya maji kuwa wabunifu na wachapakazi ili kusaidia ufikiwaji wa malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-25, kisha kukata utepe na kukabidhi pikipiki hizo.
Akisoma taarifa kabla ya zoezi la makabidhiano ya pikipiki hizo, Mhandisi Jabiri Kayilla ambaye ni Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA Mkoa wa Geita amesema mahitaji ya maji maeneo ya vijijini mkoani Geita ni lita 53,401,175 kwa siku na wastani wa uzalishaji maji ni lita 36,312,799 kwa siku hivyo upungufu ni lita 17,088,376 na huduma ya maji hupatikana kwa wastani wa 68%.
Mhandisi Jabiri ameongeza kuwa, pikipiki hizo zilipokelewa kwa ajili ya wilaya zote za mkoa wa Geita hivyo kama RUWASA wanaishukuru sana serikali na wanaahidi kuchapa kazi kwa bidii ili kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais kuwaletea wananchi maendeleo wakisema, RUWASA-Maji Bombani.
Akishukuru kwaniaba ya viongozi wa CBWSOs, Bi.Elizabeth Maige ambaye ni Mweyekiti wa Vyombo vya Kijamii vya Watumiaji Maji kutoka Nyakagwe amesema, “nampongeza sana Rais wetu mpendwa mama Samia kwani awali tulifata maji umbali mrefu, namshukuru sana na ninamsalimu kwa jina la jamhuri ya muungano wa Tanzania”
Katika tukio hilo, Katibu Tawala Mkoa Geita Prof.Godius Kahyarara aliweza kujitambulisha kwa watumishi wa RUWASA huku akiwaachia changamoto ya kuhakikisha rasilimali zilizopo Geita zinatumika vizuri kuinua uchumi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa