Mkuu wa Mkoa Geita Mhe.Martine Shigela amesisitiza juu ya utendaji kazi na watu kuepuka kugeuza dhamana kuwa mali ya familia bali kuzingatia sheria, taratibu na kanuni katika utekelezaji wa majukumu ya serikali.
Mhe.Shigela amesema hayo Januari 30, 2023 wakati akiwaapisha wakuu wa wilaya wapya watatu walioteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan Januari 25, 2023 ambapo watatu kati ya wanne ndiyo waliyokula kiapo.
“kwanza tumshukuru Mhe.Rais Dkt.Samia kwakuwa anaipenda Geita hata kuiletea watoto wenu, tena wa kutoka Geita. Hivyo muwape ushirikiano, msigeuze dhamana kuwa mali ya familia. Tuwape nafasi wafanye kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu”. Alisema RC Shigela.
Katika kuhitimisha, RC Shigela aliongeza kusema yapo mambo muhimu matatu ambayo viongozi hao wanapaswa kuzingatia akisema, “jukumu la wakuu wa wilaya linahusisha uongozi, yani ifahamike kuwa, kila kitu kinamhusu mtawala. Huwezi kutawala usilolijua, hivyo nendeni mkafanye mikutano, wasikilizeni wananchi. Na juu ya usimamizi, mambo yote yanapaswa kufanyika kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni na mwisho ni juu ya usalama, unahusu raia, mali, eneo na maisha ya watu, hivyo tatueni migogoro”
Nao kwa nyakati tofauti, Mhe.Said Nkumba DC Bukombe anayeendelea na kituo chake, Mhe.Grace Kingalame DC Nyang’hwale, Mhe. Deusdedith Katwale DC Chato na Mhe.Cornel Magembe DC Geita wamesema wanamshukuru Mhe.Rais Dkt.Samia kwa kuwaamini na kuwateuwa kuwa wakuu wa wilaya na kuomba ushirikiano kwa wananchi, watendaji huku wakiomba viongozi wa dini kuwakumbuka katika maombi.
Kwa upande mwingine, mwenyekiti wa CCM Mkoa Geita Mhe.Nicholaus Kasendamila amewaombea viongozi hao kuwa na afya njema, hekima na busara katika kutekeleza majukumu yao akiwakumbusha kuwapenda wananchi, kuwasikiliza kisha akawakaribisha mkoani Geita.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, viongozi wa dini pamoja na taasisi binafsi.
Geita ya Samia, Hakuna Kilichosimama
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa